Mara nyingi mwanaadamu akiwemo katika msafara wa maisha yake binafsi, hujikuta akiwa ni mpweke na mgeni ndani ya msafara huo. Lakini hakuna budi kila mmoja wetu kuwemo ndani ya msafara huo. Ukiizingatia vizuri njia ya msafara wako, utaikutia kuwa: ndani yake huwa mna mambo yaliyokuwa tayari yameshathibitika na kujidhatiti bila ya hiari na matakwa yako binafsi, nayo ni kama vile: kabila, familia tulizozaliwa ndani yake, uwananchi asili, kimo chetu cha urefu na upana na mengineyo. Lakini tukiangalia upande mwengine tukiwemo ndani ya msafara huo huo, tutajikuta kuwa tunakabiliwa na mambo mengine ambayo tunaweza kuyatekeleza au kuto yatekeleza kwa kupitia njia tofauti, na matendo hayo huwa yanangojea uwamuzi kutoka kwetu wenyewe ili yaweze kutendeka na kuthibiti, na hapo ndipo mwanaadamu anapoanza kujisaili na kujiuliza kuwa njia ipi aifuate na ipi aepukane katika utendaji au uepukaji wake wa mambo ya aina hiyo? Na hapo ndipo utapokabiliwa na maswali kutaka katika akili yako yanayokutaka kutoa uwamuzi sahihi kuhusiana na mambo hayo, na mfano wa maswali hayo ni kama vile: ipi? Lipi? Nini? Wapi?
Hapa tutafahamu kuwa, maneno kama vile: ipi, lipi, nini au kitu gani, ndiyo maneno yanayo kuonyesha kuwa wewe ni mwenye uhuru katika chaguo lako pale unapokabiliwa na aina ya pili ya mambo tuliyoyataja.
Kitendo cha mwanaadamu katika ulimwengu huu, hakiko nje ya matokeo yanayotokea ndani ya ulimwengu huu, na ni kawaida kuwa kila tokeo huwa linahitajia sababu kamili ili liweze kutokea, na kutokana na kuwa mwanaadamu ni sehemu ya yale yaliyomo ndani ya ulimwengu huu, na yeye hawezi kuepukana na uhusianao uliopo baina yake na baina ya vile vilivyomo ulimwenguni. Kwa kutokana na hali hiyo, mwanaadamu hatoacha kuathiriwa na vitu au matokeo mbali mbali katika utendaji wa matendo yake, naye vile vile hatokosa kuviathiri vitu vyengine vilivyomo ndani ya ulimwengu huu huku akiwemo ndani ya msafara wa maisha yake.[1] Kwa mfano, mtu anapotaka kuila tonge ya chakula, huwa anahitajia mambo tofauti ili aitimize kazi hiyo. Yeye katika kuitimiza kazi hiyo atahitajia mkono, mdomo, elimu pamoja na shauku ya kula. Na kwa upande wa pili huwa kunahitajika kuwepo chakula na kuto kuwepo vizuizi vitakavyozuia kitendo hicho kutokea, vile vile huwa kunahitajika muda maalumu na sehemu maalumu ya kutendea kitendo hicho. Na iwapo moja ya vitu hivyo vitakosekana basi tendo halitotendeka, na kama vitu hivyo (sababu tosha) vitakamilika, hapo ndipo tendo litakapotendeka.[2] Tunapolitumia neno (Sababu tosha) huwa tunamaanisha kule kukamilika kwa sababu zote pamoja na kutokuwepo vizuizi.
Ewe msomaji, fahamu kuwa: Mola wetu aliyetumiliki ametaka kumfanya mwanaadamu kuwa na hiari katika matendo yake; yaani iwapo kitu fulani kitakuwa kinahitajia aina tano za sababu ili kitengemae kwa kupitia mkono wa mwanaadamu, basi moja kati ya sababu hizo huwa ni uamuzi wa mwanaadamu wa kukitenda kitendo hicho, kwa mfano ili taa iwake kunahitajika kupita mambo tofauti. Kuwaka kwa taa huwa kunahitajia kuwepo umeme, kuwepo, swichi, waya ulioungana na chanzo cha umeme, pamoja na kuwepo mtiririko wa umeme ndani ya waya. Pamoja na yote hayo lakini bado panahitajika kuwepo mbonyezaji wa swichi, ili taa ziwake, lakini kazi hiyo huwa iko ndani ya matakwa yetu wenyewe. Huu ndiyo mfano wa yale matendo ambayo sisi tuna uhuru wa kuyatenda au kuepukana nayo, na katika matendo ya aina hii Mola Mtakatifu amempa uhuru kamili mja wake wa kubonyeza swichi ya matokeo au kuto bonyeza, amefanya hivyo ili mwnaadamu atende matendo yake kwa matakwa yake mwenyewe, hii ni katika hali ambayo mambo yote yanayosababisha kupatikana tokeo fulani huwa yako tayari, isipokuwa kilicho bakia huwa ni ile hiari ya mtu mwenyewe, ambayo huwa ndiyo hitimisho la sababu zinazoweza kukifanya kitendo fulani kukamilika. Hivyo basi iwapo swichi hiyo itapata mbonyezaji, kitendo kitatokea na asipopatikana, kitendo kitabaki bila ya kupata mtendaji. Kwa hiyo yawezekana kupatika sababu zote zinazowe kusababisha jambo fulani kutokea, lakini bila ya mtu mwenyewe kuruhusu tokeo hilo litokee, tokeo hilo halitotokea. Hii ni katika matokeo maalumu ambayo mtu mwenyewe huwa ana uwezo na uhuru ndani yake, kwa hiyo kuwepo kwa sababu maalumu si sababu ya kupatikana tokeo bila ya kuwepo matakwa ya mtu mwenyewe katika matokeo ambayo mtu ana uhuru nayo wa kuyatenda au kuepukana nayo, kwani sababu haiwezi kuitwa kuwa ni sababu kamili bila ya kupatikana matakwa ya mtu fulani yatakayoikamilisha sababu hiyo. Matakwa na hiari ndivyo vikamilishaji vya sababu za matokeo au vitendo mbali mbali. Kila mmoja mwenye akili huwa anafahamu usemi tuliyo usema bila ya kutaka ufafanuzi au kupitisha juhudi maalumu za kiakili, na hilo liko wazi kwani sisi tanawaona wata kuwa wanayatofautisha yale matende wenye uhuru nayo kama vile kula, kunywa, kutembea na mengineyo, na hawayachanganyi matendo hayo na yale matendo wasiyo na uhuru nayo kama vile: kuumwa, kupona, pamoja na kuwa na kimo cha ufupi au urefu. Aina ya mwanzo ya matendo yanaweza kukubali amri au makatazo, lakini aina ya pili ya matendo hayawezi kukubali amri au makatazo kwa sababu ya kutokuwa na uhuru nayo.
Katika zama za mwanzo za Uislamu, ndani ya madhehebu ya Kisunni kulikuwa kuna aina mbili za mitazamo kuhusiana na matendo ya mwanaadamu, mtazamo wa kwanza ulisema kuwa: matendo ya mwanaadamu ni matakwa ya Mola, na haiwezekani mtu kuwa na uhuru wala kubadilisha kitu fulani ndani yake, na mtu analazimika kutenda matendo hayo huku akiwa hana uhuru wa aina yeyote. Mtazamo wa pili uliona kuwa: mwanaadamu ni mwenye uhuru juu ya matendo yake na Mola hana mchango wa aina yeyote ule juu ya matendo hayo. Lakini mafunzo ya Ahlul-Baiyt (s.a.w) ambayo yanaonekana kuenda sawa na Qur-ani, yanasema kuwa: mwanaadamu yuko huru lakini uhuru huo una aina fulani ya mchango wa Mola mtukufu, yaani Mola amemfanya mja wake kuwa na uwezo wa kutenda kitendo fulani huku akiwa na uhuru katika utendaji wake, na hii ni ruhusa kutoka kwa Mola wake. Na ruhusa hii ndiyo mchango wa Mola kwa mja wake. Na hilo ndilo tulilolisema hapo mwanzo kuwa, tokeo huwa linahitajia kupatikana kwa sababu kamili ili liweze kutokea, na sehemu moja muhimu ya sababu hizo ni chaguo la mtu mwenyewe, na chaguo hilo huwa ndio kikamilisho cha sababu hizo.[3]
[1] Kuna aina mbili za sababu, nazo ni sababu kamili na sababu pungufu. Sababu kamili ni ile sababu tosha ambayo kuwepo kwake huwa kuna sababisha kupatikana tokeo fulani bila ya kuhitajia mchango kutoka sehemu nyengine. Na sababu pungufu ni ile sababu ambayo kuwepo kwake kunachangia kutokea tokeo fulani, na ili tokeo litokee kunahitajika kukusanyika sababu nyengine ndogo ndogo. Sabau pungufu haitoshelezi katika kuleta tokeo fulani, lakini vile vile kuto kuwepo kwake kunakuwa ni pingamizi ya kupatikana tokeo.
[2] Rejea kitabu: shia dar Islam ukurasa wa 78 cha Sayyid Muhammad Husein Tabatabai.
[3] Rejea uk: wa 79 wa kitabu kilichopita.