Imamu Husein bin Ali (a.s) ambaye ni Imamu wa tatu wa Kishia, ni mtu mwenye fadhila kubwa mbele ya Mola wake, na fadhila hizo amezipata kwa kutokana na malengo yake, matendo, kutojitanguliza mbele katika maslahi ya jamii yake pamoja na kule kujitoa keake muhanga kwa ajili ya dini na manufaa ya walimwengu wote wenye kupenda haki. Yote hayo ndiyo yaliyomfanya yeye kupata fadhila tofauti duniani na Akhera kutoka kwa Mola wake Mtukufu, na moja kati ya fadhila za duniani alizopewa, ni kule kuhimizwa Waislamu kulizuru kaburi lake, pamoja na kuwaahidi wale watakaolizuru kaburi hilo kupata ujira mkubwa usio na kifani. Na moja kati ahadi walizo ahidiwa Waislamu hao, inaonekana katika nukuu zilizonukuliwa na Sheikh Mufiid na wengineo katika Hadithi ambayo ni Mutawaatir kutoka kwa Imamu Jaafar Saadiq (a.s), isemayo: “…Na mtu atakayelizuru kaburi la Imamu Husein siku ya Ashura, fadhila zake ni kana kwamba mtu huyo amekutana na Mola wake katika Arshi ya Mwenye Ezi Mungu”. Hadithi hii inayozungumzia fadhila hizi, inafanana na ile Hadithi ya Imamu Ridha (a.s), inayozungumzia fadhila za kulizuru kaburi la Mtume (a.s.w.w), na Hadithi hiyo ni kama ifuatavyo: Imamu Ridha (a.s) alipokuwa akiwafahamisha watu maana ya kumzuru Mola alisema: “Kwa kutokana na kwamba, kumuona na kumzuru Mola ni jambo lisilowezekana, hivyo basi Mola mwenyewe amejaalia kuwa, kumzuru Mtume wake (s.a.w.w) ni sawa na kumzuru Yeye (s.w)”. Lakini sisi hapa tunatakiwa kuwa na mazingatio ya kwamba, kumzuru Imamu Husein (a.s), ni moja kati ya sababu zinazosababisha kudumu na kubakia hai malengo ya Imamu Husein (a.s), na kubakia hai huko kwa malengo hayo, ni sawa na kubakia hai kwa dini ya Mola, jambo ambalo limetiliwa mkazo na ibara mbali mbali za Qur-ani tukufu.
Uislamu ni dini ya matendo, na malipo ya matendo hayo yapo kwa Mola mwnyewe, na ujira bora zaidi juu ya matendo hayo humuangukia yule mwenye matendo yaliotimia zaida kiikhlasi, na Mola ndiye mlipaji bora kuliko walipaji wote, naye hatoupoteza ujiwa wa mtu yoyote yule miongoni mwa watendaji hao.[1] Kila nia ya mja juu ya matendo ayatendayo inapokamilika kiikhlasi, na kila mja apostahamili madhila na mitihani mbali mbali kwa ajili ya Mola wake, ndipo anapopata ujira mkubwa zaidi, na thamani yake huwa ni kubwa zaidi mbele ya Mola wake. Na msingi huo ndio uliowafanya mitume na Maimamu (a.s) kuwa na cheo kikubwa zaidi kuliko wengine mbele ya Mola wao. Imamu Husein naye (a.s) ambaye ni Imamu wa tatu wa Kishia, ni mtu mwenye cheo kikubwa mbele ya Mola wake. Cheo chake hicho hakukipata kwa sababu ya nasaba yake ambayo ni nasaba iliyoungana moja kwa moja na Mtume (a.s.w.w), bali cheo hicho amekipata kw kutokana na makusudio ya malengo aliokuwa nayo, matendo yaliyokamilika, mitihani mbali mbali pamoja na kukubali jukumu la kujitoa muhanga kwa ajili ya kuinusuru dini ya Mola wake. Yeye (a.s) pale alipokabiliana na Yazidu katika mapambano ya Karbala, hakuwa na malengo ya kidunia yaliyotokana na nafsi yake, bali malengo yake yalikuwa ni kuiokoa dini ya Mola wake, pamoja na kuirejeshea dini hiyo heshima yake iliokuwa tayari imeshaanza kupotezwa. Leo imekuwa ni jambo la wazi ka kila mwenye akili timamu kuwa, iwapo Imamu Husein (a.s) hangesimama kidete mbele ya utawala wa Banii-Umayya, basi sisi leo tungelibakiwa na jina tu la Uislamu. Leo uhakika wa dini ungelibakia kuwa ni mateka wa Banii-Umayya, na wala uhakika wa Uislamu usingeweza kutufikia sisi tunaoishi katika zama hizi. Kujitoa kwake muhanga Imamu Husein (a.s), ulikuwa ni mchanganyiko wa mapenzi na akili iliyotimia, mchanganyiko ambao uliweza kufanya kazi kisawasawa hadi kuuangusha utawala wa kidhalimu wa Banii-Umayya. Na kwa upande wa pili Imamu Husein (a.s), alielewa wazi kuwa Yeye (a.s) hana hata njia moja itakayomuwezesha kuishi, kwani Yeye (a.s) alielewa wazi kuwa lengo la Yazidu ni kumuondoa Yeye (a.s) duniani, pia alielewa namna ya unafiki wa watu wa mji wa (Kuufa) ulivyokomaa, kwani unafiki wao ulikwisha mdhihirikia yeye pale wao walipouonesha unafiki wao kwa Ali bin Abii-Taali na kwa Hassan bin Ali (a..s). Pamoja na yote hayo, lakini yeye hakurudi nyuma, bali aliikusanya familia yake na kuelea vitani bila ya khofu wala woga, naye alipigana vita hivyo kwa moyo wa ukunjufu mbele ya Mola wake, na mwishowe damu yake takatifu ikama ndiyo mbolea iliyouimarisha Uislamu na kuutoa katika unyonge.
Ingawaje kuna wengi waliouza roho zao kwa ajili ya Mola wao, lakini hakuna hata vita vimoja vilivyoweza kulingana na tokeo la Mauwaji ya Karbala, kwani hakukutokea mauwaji ya kikatila zaidi ya mauwaji hayo! Mola mtukufu katika Qur-ani anasema: “Kwa hakika Sisi tunawalipa wenye kusubiri ujira wao bila ya hesabu”![2] je Tarehe imeweza kunukuu kisa chenye mauwaji ya kigaidi zaidi ya mauwaji ya Karbala? Na je kuna mtu aliyekuwa na subra zaidi ya Imamu Husein (a.s)? Subra yake na kujitoa kwake muhanga, hakukuwa na na hata chembe moja ya kutafuta maslahi binafsi. Ni ujira gani basi utokao kwa Mola, anaostahiki mtu kama huyo kuupata.
Mwenye Ezi Mungu amempa Yeye (a.s) ujira na utukufu usio na kifani, miongoni mwa fadhila na utukuffu aliopewa na Mola wake, ni kule kuhimizwa watu kulizuru kaburi lake, huku watu hao wakiahidiwa fadhila kubwa kutoka kwa mola wao kwa yule atakayemzuru Imamu Husein (a.s). moja kati ya Hadithi zilizowaahidi watu watakaomzuru Yeye (a.s) kupata fadhila kubwa, ni ile Hadithi Mutawaatiru iliyonukuliwa na Shekh Mufiid, Hadithi hiyo ni kama ifuatavyo: Imamu Jaafar Saadiq (a.s) amesema: ““…Na mtu atakayelizuru kaburi la Imamu Husein siku ya Ashura, fadhila zake ni kana kwamba mtu huyo amekutana na Mola wake katika Arshi ya Mwenye Ezi Mungu”.[3] Na wala hakuna jambo la ajabu kuhusiana na Hadithi hii, Kwani kuna Hadithi nyingi zenye kuzungumzia aina kama hiyo ya fadhila kwa yule atakayemzuru Mtume (s.a.w.w), na Hadithi hii inayozungumzia fadhila hizi, inafanana na ile Hadithi ya Imamu Ridha (a.s), inayozungumzia fadhila za kulizuru kaburi la Mtume (s.a.w.w), na Hadithi hiyo ni kama ifuatavyo: Imamu Ridha (a.s) alipokuwa akiwafahamisha watu maana ya kumzuru Mola alisema: “Kwa kutokana kwamba, kumuona na kumzuru Mola ni jambo lisilowezekana, hivyo basi Mola mwenyewe amejaalia kuwa, kumzuru Mtume wake (s.a.w.w) ni sawa na kumzuru Yeye (s.a)”.[4]
Lakini hapa tunatakiwa kuwa na mazingatio ya kwamba, kumzuru Imamu Husein (a.s), ni moja kati ya sababu zinazosababisha kudumu na kubakia hai malengo ya Imamu Husein (a.s), na kubakia hai huko kwa malengo hayo, ni sawa na kubakia hai kwa dini ya Mola, jambo ambalo limetiliwa mkazo na ibara mbali mbali za Qur-ani tukufu.
[1] Suratu Aalu-Imraan Aya ya 171. Suratut-Tawba Aya ya 120.
[2] Suratuz-Zumar Aya 10.
[3] Na maandiko ya Hadithi hiyo ni kama ifuatavyo:
- جَعْفَرُ بْنُ مُحَمَّدِ بْنِ قُولَوَيْهِ فِي الْمَزَارِ عَنْ جَعْفَرِ بْنِ مُحَمَّدِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ الْمُوسَوِيِّ عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ نَهِيكٍ عَنِ ابْنِ أَبِي عُمَيْرٍ عَنْ زَيْدٍ الشَّحَّامِ عَنْ جَعْفَرِ بْنِ مُحَمَّدٍ ع قَالَ مَنْ زَارَ الْحُسَيْنَ ع لَيْلَةَ النِّصْفِ مِنْ شَعْبَانَ غَفَرَ اللَّهُ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ وَ مَا تَأَخَّرَ وَ مَنْ زَارَهُ يَوْمَ عَرَفَةَ كَتَبَ اللَّهُ لَهُ أَلْفَ حَجَّةٍ مُتَقَبَّلَةٍ وَ أَلْفَ عُمْرَةٍ مَبْرُورَةٍ وَ مَنْ زَارَهُ يَوْمَ عَاشُورَاءَ فَكَأَنَّمَا زَارَ اللَّهَ فَوْقَ عَرْشِهِ.
[4] Rejea kitabu (Tah-dhiibul-Ah-kaam), juz/6, uk/3. Na maandiko ya Hadithi hiyo ni kama iffuatavyo:
قاْلِ الصَّادِقِ ع مَنْ زَارَ رَسُولَ اللَّهِ ص كَمَنْ زَارَ اللَّهَ فَوْقَ عَرْشِهِ ؛ وسائلالشيعة ج : 14 ص : 335،حدیث 19340، وَ عَنْ عِدَّةٍ مِنْ أَصْحَابِنَا عَنْ سَهْلِ بْنِ زِيَادٍ عَنْ مُحَمَّدِ بْنِ الْحُسَيْنِ عَنْ مُحَمَّدِ بْنِ إِسْمَاعِيلَ عَنْ صَالِحِ بْنِ عُقْبَةَ عَنْ زَيْدٍ الشَّحَّامِ قَالَ قُلْتُ لِأَبِي عَبْدِ اللَّهِ ع مَا لِمَنْ زَارَ رَسُولَ اللَّهِ ص قَالَ كَمَنْ زَارَ اللَّهَ فَوْقَ عَرْشِهِ الْحَدِيثَ.