1- Suala la Malaika kuumbwa kutokana na nuru ya watu fulani, ni suala maarufu lilinukuliwa kutoka kwenye Riwaya za pande zote mbili, za Masunni na Mashia. Ndani ya vitabu vya Kishia, kuna Riwaya zinazoelezea kuwa: Malaika wameumba kutokana na nuru za watu maalumu, kama vile: Mtume na Maimamu (a.s), au kutokana na nuru nyengine mbali mbali. Pia kuna Riwaya zinazopatikana ndani ya vitabu vya Masunni, zisemazo kuwa: khalifa wa kwanza ameumbwa kutokana na nuru ya Mtume (s.a.w.w). Kuonekana kwa aina kama hii ya Riwaya kutoka pande zote mbili za Kisunni na Kishia, huwa hakutoi bishara inayo onesha kuwa Waislamu wa pande mbili hizo wote kwa pamoja, ni wenye kuamini kisawa sawa suala hilo. Pia ndani ya vitabu vya Kishia kuna Riwaya zinazosema kuwa: Mashia wameumbwa kutokana na mabaki ya udongo wa Maimamu (a.s). Lakini kupatikana kwa aina mbali mbali za mitazomo kuhusiana na namna ya ukamilikaji wa maumbile ya wafuasi au viongozi wa makundi mbali mbali ya Waislamu, huwa inatokana na fikra na mitazamo mbali mbali kuhusu mjengeko mzima wa ulimwengu pamoja na malengo ya kuumbwa kwa ulimwengu huu yalivyo.
2- Kuwepo kwa Malika wanao omboleza na kumlilia Imamu Husein (a.s), pamoja na wale Malaika wanaokuja kwa ajili ya kulizuru kaburi lake (a.s), ni jambo lililomashuhuri ndani ya vitabu vya Mashia, na pia kuna Riwaya zinazolizungumzia suala hilo kwa namna moja au nyengine ndani ya vitabu vya Kisunni, kwa hiyo suala hilo si suala lenye utata mkubwa mbele ya Waislamu wasiokuwa na kasumba, wa madhehebu mbali mbali.
Nyenzo na fani za kila mmoja miongoni mwa wanazuoni wa madhehebu mbali mbali ya Kiislamu, huwa ndiyo durubini muhimu ya kuyapeleleza na kuyafanyia uchunguzi maumbile halisi ya ulimwengu huu yalivyo, kila mmoja kati ya wanazuoni wa madhehebu ya mbali mbali ya Kiislamu, hufuata njia maalumu katika kuzifahamu Riwaya na Aya mbali mbali. Moja kati ya njia hizo, ni kuzitupia macho Riwaya Aya hizo, kisha kutoa hukumu kwa jinsi tu ya udhari wa Aya na Riwaya hizo zilivyo, bila ya kuzitafakari na kuzifanyia uchunguzi kwa makini. Na kuna njia nyengine zinazotumiwa na baadhi ya wanamadhehebu wengine, ambazo ni kinyume na ile njia ya mwanzo tuliyo ifafanua, na miongoni mwazo ni: njia ya kutumia akili tafakuri, Falsafa, na Irfani. Bila shaka yeyote yule atayetaka kufasiri Riwaya au andiko fulani kutoka katika kitabu fulani, ni lazima aanguke (apite) kwenye moja kati ya njia hizo tulizozitaja. Hivyo basi kila mmoja miongoni mwa: Wana-Falsafa, Wana-Akida na Wana-Irfani -katika zama zote zilizopita- huwa ni wenye mitazamo yenye kutofautiana juu ya hali nzima ya kimaumbile inayodirikiwa na wanaadamu ndani ya ulimwengu huu. Dalili hasa za kutofautiana kwa mitazamo yao, ni zile njia na nyezo zinazotumiwa na kila mmoja wao. Kwa hiyo kila mmoja miongoni mwao, hutoa picha maalumu kuhusiana na sauala la uumbaji. Mtazamo usemao kuwa: uumbaji wa ulimwengu huu umepita katika hatua kumi tofauti zijulikanazo kwa jina la (Akili kumi), ni mtazamo uliokuja kutoka kwa Wana-Falsafa, na ule mtazamo wa kutafuta maana mbadala katika kuzifasiri baadhi ya Hadithi, ni mtazamo wa wale wenye kutumia (akili tafakuri). Hivyo basi yeyote anayetaka kulifahamu suala la uumbwaji wa Malaika, ni lazima azielewe tofauti za kila moja kati ya njia zinazofuatwa na wanazuoni mbali mbali. Pia mara kwa mara sisi tumekuwa tukitoa tahadhari na kuwazindua watu ya kuwa: si kila Hadithi iliomo ndani ya vitabu vya Shia na Sunni huwa ni sahihi. Na usahihishaji wa Riwaya hizo uko juu ya shingo za wanazuoni, na tayari wanazuoni wa Kishia na Kisunni, wameshazipanga Hadithi katika matabaka mbali mbali, na hadi leo wanazuoni wa Kisunni wameweza kutayarisha vitabu maalumu vilivyozikusanya Hadithi sahihi kupitia mitazamo yao, na vitabu hivyo huitwa (Sihahi Sitta).
Baadhi ya Riwaya za Kisunni na Kishia zinaashiria kuwepo kwa nuru ya Mtume (s.a.w.w), kabla ya kuumbwa kwa dunia.[1] Pia kumepokewa Hadithi kutoka kwenye vitabu vya Kisunni, isemayo kuwa: khalifa wa kwanza ameumbwa kutokana na nuru ya Mtume (s.a.w.w), na khalifa wa pili yeye pamoja na Aisha, wameumbwa kutokana na nuru ya Abu-Bakar….[2] Vile vile ndani ya vitabu vya Kishia, kuna Riawaya zinazo onekana kuripoti kuwa: Malaika wameumbwa kutokana na nuru ya Mtume na Maimamu (a.s), na wakatiki mwengine hunukuliwa Riwaya zisemazo kuwa: Malaika wameumbwa kutokana na nuru nyengine zisizokuwa hizo. Haipasi mtu kuzikubali au kuzikataa moja kwa moja aina kama hizo za Riwaya, bali ni wajibu wa kila mmoja wetu kuzitafakari kwa makini zaidi.
La sahihi kuzingatiwa ni kwamba: iwapo mtu atataka kuzifahamu itikadi halisi za Kishia, itambidi kusoma vitabu maalumu vilivyoandikwa na wanachuoni wa Kishia kwa ajili ya kuzibainisha itikadi zao. Si dhana nzuri kwa wasomaji kuzisoma baadhi ya Hadithi zilizomo ndani ya vitabu vya Kishia, kisha kuanza kuwavurumishia tuhuma mbali mbali, kwani kuna Riwaya mbali mbali ndani ya vitabu vya Kishia, ambazo wanazuoni hawakubaliani nazo kwa kutokana na sababu mbali mbali. Vile vile kuna Riwaya nyengine zilizopokelewa kupitia njia moja tu, Riwaya ambazo huwa si tegemeo jema la mtu kujijengea itikadi maalumu za kidini. Kupatikana baadhi ya Riwaya zisemazo kuwa: Malaika wameumbwa kutokana na nuru ya Maimamu, au khalifa wa kwanza ameumbwa kutokana na nuru ya Mtume (s.a.w.w), au Riwaya zenye kufanana na hizo ndani ya vitabu vya Kisunni na Kishia, hazimaanishi kuwa Masunni na Mashia wote ni wenye kuamini suala hilo. Ingawa imani hiyo haiwezi kumtoa mtu kwenye Uislamu, lakini bado suala hilo litabakia kuwa ni suala walilotofautiana Waislamu juu ya uhakika wake, kama vile walivyokhtalifiana katika suala la uhakika wa sifa za Mwenye Ezi Mungu.
Ama kuhusiana na aina ya pili ya suala lako lenye kuhusu kilio na maombolezo ya Malaika kwa ajili ya Imamu Husein (a.s), pamoja na suala la Malaika hao kuja kwa ajili ya ziara maalumu ya kaburi lake (a.s), inabidi kuzingatia mazingatio yafuatayo:
1- Ndani ya vitabu vya pande zote mbili za Kisunni na Kishia, kuna Hadithi zinaelezea kuwa: Malaika huwa wanawafurahia na kuwalilia baadhi ya watu maalumu.[3] Sisi hapa tutazifafanua Riwaya hizo bila ya kuchunguza aina na namna ya uliaji wa Malaika hao.
Katika zama zilizopita kabla ya Uislamu, kunaonekana kuwepo kwa ibabara zinazofafa na hii ya Malaika kuwalilia watu fulani, na miongoni mwa ibara hizo ni: kilio cha mbingu, ardhi, kupatwa kwa jua na kulia kwa upepo kwa ajili ya watu fulani waliofariki au kuuliwa, na pia Qur-ani imeliashiria suala hilo.[4] Na muda si mrefu ujao, tutalifafanua suala kulia kwa mbingu na ardhi lililozungumziwa ndani Qur-ani, ambapo baadhi ya wafasiri wa Qur-ani wanaamini kuwa: kulia kwa mbingu na ardhi huwa kunamaanisha kule kulia kwa Malaika walioko mbinguni na wanaadamu wanaoishi juu ya ardhi hiyo. Pia suala hili linaonekana wazi ndani ya maandiko ya dini ya Kiislamu. Vitabu vya pande zote mbili vinalinukuu suala hilo, kwa hiyo hili si suala linalo onekana kuwa na utata miongoni mwa wafuasi wa dini hii.
Ili suala hili liweze kuwa wazi kwa muulizaji wetu, sisi hapa tutazinukuu aina zote mbili za Riwaya zinazolinukuu suala hili, na Riwaya hizo ni kama ifuotavyo:
1- Kutoka Mtume (s.a.w.w) tunanukuu Riwaya isemayo: “Hakuna hata muumini mmoja atakayekufa mpweke (asiye na mtu wa kumlilia), isipokuwa muumini huyo ataliliwa na mbingu na ardhi.”[5] Pia kuna Riwaya iliyokuja kwa mtindo na maneno hayo hayo, isipokuwa badala ya neno mbingu na ardhi, wametajwa Malaika ndio watakao mlilia mtu huyo.[6]
2- Riwaya nyengine zinasema kuwa: “Pale Adam Alipofariki, alililiwa na viumbe wote wa ulimwenguni, na kilio hicho kiliendelea kwa muda wa siku saba.[7]
3- Kutoka katika maneno ya Mtume (a.s.w.w), kuna Hadithi isemayo kuwa: siku moja Mtume (s a. w.w.) alikutana na kijana mmoja ambaye ni mcha-Mungu sana, aliyekua akilia mno kwa ajili ya mapenzi ya Mola wake, kilio ambacho kiliwaliza hata Malaika, Yeye (s.a.w.w) alimsogelea na kumwambia: “Kwa hakika kilio chako kimewafanya hata Malaika kulia”.[8]
4- Pia moja kati ya Hadithi muhimu kuhusiana na jambo hili, ni ile Hadithi ya Mtume (s.a.w.w), inayowazungumzia wapiganaji jihadi. Baadhi ya maneno yaliomo ndani ya Hadithi hiyo, yanasema kuwa: “pale familia zao zinapoagana nao, kuta za nyumba za wanajihadi hao huwa zinawalilia.[9]
5- Katika tafsiri ya Qurtubiy imeelezwa kuwa Aya isemayo “ما بکتهم السماء ...” yenye kuashiria kuwa: wale wailioangamizwa na Mola wao, hawakuliliwa na mbingu wala ardhi, haikusudii kuelezea kilio cha mbingu ardhi, bali kinachokusudiwa ni kilio cha Malaika, na usemi huo wa Qur-ani umefanana na ule usemi wa ndugu wa nabi Yusuf (a.s) uliosema “و اسال القریه” (na nendeni mkakiuluze kijiji), wenye kumaanisha watu wanaoishi ndani ya kijiji hicho, na sio kijiji chenyewe, kwani kijiji hakisemi. Pia Qurtubiy ameinukuu Riwaya kutoka kwa Mtume (s.a.w.w), isemayo kuwa muumini anapofariki huliliwa na mbingu na ardhi kwa muda wa siku arubaini.[10]
Vile vile kuna Riwaya nyingine zinazo elezea furaha ya Malaika kwa ajili ya watu maalumu, na miongoni mwa watu waliotajwa kuwa Malaika huwa ni wenye kuwafurahia, ni khalifa wa mwanzo,[11] na khalifa wa pili pale aliposilimu[12], pia imenukuliwa kuwa Malaika waliifurahia sana roho ya Saad bin Maadh, na hata Arshi ilitetemeka kwa furaha.[13]
Hii ni sehebu ya jawabu ya swala lako, pia sisi hatutoacha kulizungumzia suala la kuteremka Malaika, ambayo ni sehemu ya pili ya swala lako, ingawaje kwa kuepuka kuwachosha wasomaji wetu inatubidi kulizungumzia jambo hilo kwa mukhtasari tu.
Miongoni mwa Riwaya na Aya zinazoligusia suala hili, zimelifafanua hilo katika matokeo tofauti, kama vile msaada wa Malaika walioteremka kwa ajili ya vita vya Badr[14], au kushuka kwa Malaika kwa ajili ya kumkosha Handhala, kushuka kwao na kulibeba jeneza la Saad bin Maadh.[15]
Jambo muhimu zaidi katika makala hii, tulilolichambua kupitia Aya na Hadithi mbali mbali, ni suala la Malaika kumlilia Imamu Husein (a.s), vitabu vya Kisunni vimenukuu Hadithi nyingi sana kuhusiana na hilo, ingawaje Hadithi hizo zinaonekana kuwa na baadhi ya tofautia kidogo katika ufikishaji wake wa maana, lakini tofauti hizo hazionekani kuuvunja uhusiano wa kimaana uliomo baina yake. Pia kuna Riwaya zilizonukuliwa na Mashia kutoka kwa Mtume na Maimamu (a.s), ambazo zinafanana na zile zilizonukuliwa kutoka kwa Masunni. Baadhi ya wapokezi wa Riwaya hizo ni: Sa’adiy, Qurra bin Khaalid, Mujaahid na wengineo, na moja kati ya Riwaya hizo, ni ile Riwaya iliyokuja kwa mtindo wa maneno yafuatayo: “Palae Husein bin Ali (a.s) alipouwawa, basi mbingu na ardhi zilimlilia, na alama za kilio hicho, ni ile alama maalumu ya rangi nyekungu ilio onekana mbinguni.[16]
Baadhi ya Riwaya zitokazo kwa Mashia zinazohusiana na jambo hili ni kama ifuatavyo:
Imepokelea Hadithi kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) kuwa: Malaika huwa wanapita katika vikao vyenye kutajwa utajo wa Mola Mtakatifu, nao hushiriki katika utajo huo, pia wao hulia pale wanapolia watu wa vikao hivvyo.[17] Ndani ya Riwaya hii mmezungumzwa vitu viwili, navyo ni kilio cha Malaika pamoja na hudhurio lao.
Kutoka kwa Imamu Kaadhim (a.s) kumepokelewa Hadithi isemayo kuwa: “Endapo muumini atafariki, basi Malaika huwa ni wenye kumlilia, pia maeneo yote ya ardhi ambayo yeye aliyatumia kwa ajili ya kumuabudu Mola wake yatakua ni yenye kulilia muumini huyo”.[18]
Iwapo sisi tutazizingatia Riwaya hizi kwa makini, tutapata kufahamu mambo mawili ndani yake:
1- Yaliyozungumzwa ndani ya Riwaya hizi ni: kilio cha viumbe mbali mbali, wakiwemo Malaika, ardhi pamoja na mbingu.
2- Kuteremka kwa Malaika kwa ajili ya kuwasaidia na kuwaunga mkono watu maalumu, kama vile wanajihadi, waumini, masahaba pamoja na mashahidi.
Ufafanuzi uliotolewa utakuwa umashaweka wazi uhakika wa Malaika kuwalilia baadhi ya watu maalumu. Kwa hiyo hatufikirii kuwa bado litakuwa ni jambo geni lenye kushangaza kusemwa kuwa Imamu Husein (a.s), ni mmoja kati ya wale wenye kuliliwa na Malaika, kwani Yeye (a.s) ni mwenye sifa zote za wale waliotajwa kuliliwa na Malaika ndani ya Riwaya mbali mbali zilizopita.
Imamu Husein (a.s) ni mjukuu wa Mtume (s.a.w.w), pia Yeye ni miongoni mwa watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w).[19] Na Mtume (s.a.w.w) amesema kuwa: “Hassan na Husein ni mambwana wa vijana wa peponi”.[20] Sifa alizonazo Husein bin Ali (a.s), ni sifa maalumu zisizoweza kupatikana na mtu au sahaba mwengine zaidi yake, isipokuwa sifa kama hizo unaweza kuziona kwa watu wa nyumba ya Mtume tu (s.a.w.w).
Jihadi ya Imamu Husein (a.s) dhidi ya serikali ya Yazidu iliyokuwa na nia ya kuupotosha Uislamu, ilikuwa ni jihadi moja kuu jihadi ambayo hatimae ilimsababishia Yeye (a.s) kuuwawa. Malengo ya jihadi hiyo iliyokuwa ni kuamrisha mema na kukataza maovu. Jihadi dhidi ya Yazidu imebaki kuwa ni medali moja muhimu yenye thamani iliong’aa kwenye shingo ya tarehe. Kumuabudu kwake Mola kwa utulivu na umakini, ilikuwa ndiyo sifa kuu iliyo onekana ndani ya maisha Yake (a.s), hasa pale mauti yalipomkaribia.
Lipi basi la kuwashangaza watu, pale wanapowaona baadhi ya Waislamu kumlilia Imamu Husein (a.s), au wanaposikia baadhi ya nukuu zisemazo kuwa: Maliaka wa Mwenenye Ezi Mungu ni wenye kulizuru kaburi lake kwa idhini ya Mola wao? Kwa nini wao hawashangai kusikia kisa cha Malaika waliokuja siku ya mazishi ya Sa’ad bin Maadh?
Suala hili linataka katafakariwa kwa makini zaidi, na pia linataka uchambuzi mwema zaidi, kwani kuna dalili mbali mbali, za kiakili zinazoweza kulithibitisha hilo, na pia kuna dalili nyengine kotoka kwenye Hadithi za Mtume (s.a.w.w), zinazoweza kulishibisha dalili suala hili, lakini kwa kutokana na kukhofu kurefuka mno mada hii, tumeamua kufikia hapa. Tunatarajia ufafanuzi wetu utaboresha elimu za wasomaji wetu.
[1] Ruhil-Bayaan, cha Ismail Haqqiy, juz/2, uk/370, chapa ya Darul-Fikril-Arabi, Beirut, Lebanon. Tafsiru gharaaibil-Qur-an-wa-raghaaibil-Furqaan, cha Hassan bin Muhammad Niishaabuuriy, juz/2, uk/407, chapa ya kwanza ya Daarul-kutubil-ilmiyya, Beirut, Lebanon, mwaka 1416 Hijiria.
[2] Kaashiful-bayaan-an-tafsiiril-Qur-an, cha Ahmad bin Ibrahim Tha’alabiy, juz/7, uk/111, chapa ya kwanza ya Daaru-ihyaai-turathil-Arabiyya, mwaka 1422 Hijiria.
[3] Imamu Husein (a.s) shakhsiyyate usturei, uk/143 hadi 155.
[4] Suratu Dukhaaan, Aya ya 29.
[5] Al-kaashif-an-haqaaiqit-tanziil, cha Mahmuud Al-Zamakhshariy, juz4, uk/274, chapa ya tatu ya Daarul-kutubil-Arabiy, Beirut, Lebanon, mwaka 1407 Hijiria.
[6] Nazhatul-majaalis, cha Al-Safuuriy, juz/1, uk/207, chapa ya Al-Az-hariyya, Cairo, mwaka 1346 Hijiria.
[7] Durrul-manthuur-fii-tafsiiril-maathuur, cha Jalaalud-Diin Suyutiy, juz/1, uk/162, kilichoko kwenye maktaba ya Ayatu-Llahi Mar-ashiy Najafiy, Qum Iran, mwaka 1404 Hijiria.
[8] Al-kashfu-Wal-bayaan-An-tafsiril-Qur-an, juz/9, uk/188, chapa ya Daaru-ihyaa-turathil-Arab, Beirut Lebanon, chapa ya kwanza ya mwaka 1422 Hijiria.
[9] Rejeo iliopita, juz/3, uk/206.
[10] Al-jaamiu-li-akaamil-Qur-an, cha Muhammad bin Ibrahim Shamsud-Diin Qurtubiy, juz/16, uk/140, chapa ya kwanza ya Nasir Khosro, Tehran, mwaka 1364 Shamsia.
[11] Taariikhu Madinatu Demeshq, cha Inbu Asaakir Ali bin Hassan, juz/79, uk/353, chapa ya Daarul-Fikri, Beirut, mwaka 1415 Hijiria.
[12] Tabaqaatul-Kubra cha Muhammad bin Saad Zahriy, juz/3, uk/205, chapa ya kwanza ya Daaru Saadir, Beirut, mwaka 1968 Miladia.
[13] Al-Jaamiu-li-ahkaamil-Qur-ani, juz/7, uk/304.
[14] Suratu Aalu-Imraan, Aya ya 125.
[15] Tabaqaatul-Qubra, juz/3, uk/428, chapa ya kwanza ya Daaru Saadir, Beirut, mwaka 1968 Miladia.
[16] Tafsirul-Qur-anil-Adhim, cha Ismail bin Kathiir Demeshqiy, juz/7, uk/234, chapa ya kwanza ya Daarul-Kutubil-Ilmiyya, Beirut, mwaka 1419 Hijiria. Pia rejea Durrul-Manthuur-Fii-Tafsiiril-Maathuur, juz/4, uk/264. Al-jaamiu-Li-ahkamil-Qur-an, juz/11, uk/220. Al-Kashfu-Wal-Bayan, juz/8, uk/353. Ruhul-Bayan, juz/8, uk//413.
[17] Wasaailu-Shia, cha Muhammad bin Hassan Hurrul-Aamiliy, juz/7, uk/231, chapa ya Aalul-Bait-li-ihyaai-turath, Qum, Iran, mwaka 1409 Hijiria.
[18] Al-Kafi cha Muhammad bin Yaaqub Koleiniy, juz/1, uk/38, chapa ya nne ya Darul-Kutubil-Ilmiyya, Tehran, mwaka 1365 Shamsia.
[19] Tafsirul-Qur-anil-Adhim, juz/2, uk/367.
[20] Durrul-Manthuur, juz/4, uk/263..