Please Wait
10822
Tukizingatia aina mbali mbali za tafsiri kuhusiana na Aya hii, tutaona kuwa kuna kauli tano tofauti zilizotajwa katika kuifasiri Aya hiyo, na kauli sahihi ni ile isemayo kuwa Aya hii imebeba ujumbe kwa ajili ya walimwengu usemao kwamba: dini ni jambo la kiimani
na kimoyo, na haiwezekani mtu kukalifishwa katika jambo hilo, bali mja ni kiumbe huru mwenye hiyari katika matendo yake yote ya dhahiri na ya moyoni. Hii nayo ni dalili wazi ya kuwajibu wale wajulikanao kwa jina la “Jabriyyuun” wenye kuitakidi kuwa: “mwanaadamu hana hiyari ya chaguo la imani wala hiyari ya kutenda alitakalo”. Na tukishikamana na Aya zinazoifuatia Aya iliopita, ambazo ziko katika Suratul-Baqara baada ya Ayatul-Kursiy, tutapata fimbo ya kuwarudi pia wale wanaojulikana kwa jina la (Mufawwidhuun), wenye kusema kuwa: “Mola alipokwisha kumuumba mja wake, alimpuruzia kamba ya kutenda alitakalo huku Mola akiwa amekaa chonjo bila ya kuchangia chochote ndani ya matendo yake”. Lakini hilo halikubaliki kwani Aya zinazofuatia baada yake, zinaonyesha kuwa utawala wa Mola na nidhamu yake umekikusanya kila kitu ndani ya milki na kudra yake isioepukika. Kwa hiyo haiwezekani Mola kuto kuwa na mchango wa aina fulani .
Kama ilivyokuwa imani ni kitu cha hiyari, vile vile ni kitu kisichowezekana mtu kuwa nje ya milki na kudra ya Mola Mtukufu, bali kwa kupitia misngi maalumu ya nidhamu ya Mola, Yeye huwaongoza wale wanaompa mgongo Shetani na kumuelekea Mola wao, na hilo hutendeka kwa kupitia vyanzo na sababu maalumu walizoshikamana nazo kwa hiyari zao wenyewe. Na iwapo watampa mgongo Mola wao kwa kuzikanusha dalili za haki na kumuelekea Shetani, Mola huwa haifungi milango ya shari wanayoifungua, na elewa kuwa kufunguka au kufungika kwa milango hiyo kunahitajia idhini ya Mola Mtukufu, na yote hayo yamo ndani ya milki yake. Kwa hiyo hakuna kinachotendeka bila ya kupata idhini ya Mola Mtukufu. Na hili ndilo linaloonekana katika kauli itokayo kwa Maimamu (a.s) isemayo:
“لاجبر و لاتفويض بل امر بين الامرين”
yaani “matendo ya mtu si makalifisho wala si mapuruzio ya moja kwa moja bali yako katika hali ya kati na kati”
Qur-ani inasema hivi: “Hakuna makalifo katika kuikubali dini, kwani kwa yakini uongofu na upotovu vimeshakua bayana, basi atakayemkataa Shetani na kumuamini Mola Mtukufu, kwa yakini huyo atakuwa ameshikamana na hoja (njia) madhubuti zisizopwaya, na Mola ni mwenye kusikia na ni Mjuzi”[1]
Kabla ya kupata ufafanuzi wa Aya hii, kwanza pokea nukta zifuatazo ikiwa ni kama utangulizi:
1: Maana ya maneno:
“Makalifisho” maana yake ni kumlazimisha mtu kutenda au kukubali kitu kwa lazima.
“uongofu” maana yake ni: njia iliyo sawa, kuuelekea ukamilifu wa mafanikio halali kisheria,[2] na kinyume yake ni neno “upotovu” likimaanisha kuingia katika njia ya maangamio,[3] Allaama Tabaatabai amesema: neno “uongofu” lina maana ya kuufikia ukweli na uhakika wa jambo fulani au kuwa uko njiani katika kuufukia uhakika huo, na kinyume chake ni “upotovu”. Hivyo basi neno “uongofu” na “upotovu” ni maneno yaliobeba maana pana zadi na wala hayamaanishi tu maana hizo tulizozitaja.[4]
2: Kauli za wafasiri wa Qur-ani:
Kiujumla jamala kuna kauli tano za wanatafsiri katika ufafanuzi wa Aya isemayo:
“لا اكراه فى الدين” nazo ni kama ifuatavyo:
A: Aya hii imekuja kuwakataza waislamu kuwasema wale waliosilimu vitani kuwa: “kusilimu kwao hakutokani na hiyari zao bali kutokana na msukumo wa kivita” [5].
B: Wengine wamesema kuwa: “Aya hii inawahusu Ahlul-kitabi, ya kuwa baada ya wao kukubali kutoa fidia ya kuishi kwenye ardhi ya waislamu, hapo basi waislamu hawatakiwi kuwalazimisha kusilimu”.[6]
C: Kauli nyengine ni kwamba: “Aya hii inawahusu makafiri wote, lakini Aya hii imepikuliwa (imefutwa) kwa kupitia Aya iliyoamuru vita[7] na jihadi” [8], [9].
D: Pia kuna kauli isemayo kuwa: “Aya hii inawahusu watu maalumu miongoni mwa Ansari” [10], huku wakisema kuwa Aya hii imeshuka kuwahusu watu hao, na wametaja visa mbali mbali kuhusiana na hilo, miongoni mwa visa hivyo ni kile kisa cha Ansari aliyekuwa na mtumwa wa Kiafrika aliyekuwa akimlazimisha mtumwa huyo kuukubali Uilsamu, na hapo ndipo iliposhuka Aya hii.
E: Na wengine wakasema kuwa: “Aya hii haikumshukia mtu yeyote yule, bali Aya hii ni yenye kutoa ujumbe kwa kila mtu.” Wao wanasema kuwa: “dini ni suala la kimoyo na kibinafsi, hivyo basi suala hili haliwezi kukubali makandamizo ya ulazimishaji, na kila mmoja yuko huru na mwenye hiyari katika hilo. Na hii ndiyo kauli yenye nguvu iliyokubaliwa na wanazuoni walio wengi, na hata wanazuoni wa hivi sasa ni wenye kukubaliana na kauli hii.[11]
Kinachoonekana ni kwamba kauli hii ya mwisho ndiyo kauli anayoingia akilini zaidi. Na hapa twaweza kusema kuwa: “Qu-rani imeweka wazi kabisa, kuwa: kila mmoja ana haki ya kuwa na huru wa kiimani na kiakida na wala hakuna mtu mwenye ruhusa ya kumlazimisha mwenziwe kuingia katika Uislamu kwani kila kitu kiko wazi” kwa hiyo mwenye kutaka uongofu na mwenye kutaka upotovu wote wawili wako huru. Kwa msingi huu basi matakwa ya kila mmoja yatakua na muelekeo wa chaguo lake mwenyewe. Ingawaje Aya hii inahusiana zaidi na upande wa kiimani, lakini haijifungi tu kwenye upande huo tu bali Aya hii ni yenye matumizi katika nyanja tofauti, kama vile nyanja za kisiasa, kiuchumi n.k.
Aya zilizoitangulia Aya hii na zilizokuja baada yake, zimetoa ufafanuzi wa wazi kabisa kuhusiana na masuala ya kiakida, na iwapo mtu atakua si mpinzani wa kuutambua ukweli, basi itakua ni rahisi sana kwake kuufahamu na hatimae kuukabili ukweli huo, lakini kwa kawaida siku zote huwa kuna watu wenye maradhi ya upinzani wa kiholela usio na dalili ziingiazo akilini, hilo basi ndilo lililoifanya Qurani kutumia lugha ya mkato kwa watu wa aina hiyo.
Aya hii na Aya inayofuatilia baada yake imekuja kusimamisha msingi madhubuti uliozifunga njia za wapinzani wa aina hiyo. Aya hii vile vile ni kipigo dhidi ya wale wanaodai kuwa: “mwanaadamu hana uhuru bali matendo yake ni yenye kupewa msukumo wa nguvu kutoka kwa Mola Mtukufu”,[12] hali ya kwamba ukweli sio huo kwani Mola si mwenye kumkalifisha mtu. Vile vile Aya hii itakua ni jawabu tosha juu ya wale wasemao kua: Mola amemuumba mja wake na kumuacha huru mja huyo atende alitakalo baada ya yeye kuwa tayari ameshambainishia njia iliyo sawa na ile isiyo sawa, kwa hiyo ili waja waweze kuongoka ni lazima tuwatumilie nguvu za kuwasilimisha kwa nguvu! Ili wasalimike na kupotea”. Lakini Aya hii inaukataa usemi huu, kwani ulimwengu huu ni uwanja wa mitiahani, na kila mmoja anatakiwa kuupokea mtihani wake na kuutatua kwa hiyari yake mwenyewe bila ya kulazimishwa, kwani kumlazimisha mtu jambo fulani ni kwenda kinyume na matakwa ya Aya hii.[13]
Pia Aya hii inaeleza wazi kua: uhuru wa kimatendo kimatendo haumaanishi kuwa mtu tayari ameshakuwa nje ya uwezo wa Mola wake, bali ukizingatia Aya zilizofutia baada yake, utafahamu kuwa: hakuna kitu chochote kile kinachoweza kutoka nje ya ufalme wa Mola wetu. Ufafanuzi wa Aya hizi unaonesha kuwa: kushikamana na uongofu ni kushikamana na zile sababu zinazomfanya mtu kuwa katika njia ilionyooka, na kutoshikamana na uongofo ni kujikusanyia sababu za kumtokomeza mtu katika matatizo. Na yote hayo yamepangwa na Mola kwa kupitia mpangilio maalumu wenye nidhamu iyendayo sawa na hali halisi ya mambo yalivyo.
Natija ya mwisho unayotakiwa kuielewa ni kwamba: endapo utashikamana na njia moja wapo kati ya njia mbili hizi, bila shaka hutakua na budi ya kuyakubali matokeo yatakayozaliwa kutokana na chaguo lako, na hapo hutakuwa huru katika kukubaliana au kuto kubaliana na matokeo hayo, kwani kila natija huwa inaendana na sawa na mbegu ulioiatika katika shamba la imani yako.
Wabillahi taufiq.
[1] Suratul-Baqara Aya ya 256.
[2] Kamusi ya Qur-ani juz: 3, uk: 100 ya Qurashiy Sayyid Ali Akbar.
[3] Kitabu kilichopita juz: 5, uk: 131.
[4] Tafsiri Al-miizaan, juz: 2 uk: 342.
[5] Tafsiri Majma’al-bayaan ya Tabarsiy juz: 2, uk: 126, pia Tafsiri Razi ya Abul-Futuhu Razi, juz: 2, uk: 330.
[6] Tafsiri A’amiliy ya Ibrahim A’amiliy, juz: 1, uk: 516 na uk: 515. Pia Tafsiri Majma’al- Bayaan, vile vile Tafsiri Al-Kashaaf ya Zamakh-shariy, juz: 1, uk: 487.
[7] Aya ya 5, Suratu Tawba.
[8] Suratu Tawba Aya ya 73.
[9] Rejea Tafsiri Majmaul- Bayaan na Tafsiri A’amiliy.
[10] Rejea Majmaul- Bayaan na Al-Kashaaf pia Tafsiri Nemune ya Makaarim Shirazi, Juz: 2, uk: 280 na uk: 279.
[11] Rejea Tafsiri Al- Mizan, Al- Kashaaf, na Tafsiri Nemune.
[12] Atyabul-bayaan fi tafsiri-Qur-an/ juz: 3/ uk: 18.
[13] Rejea Tafsirul-kabir ya Fakhrur-Raziy/ juz: 3/ uk: 15.