advanced Search
KAGUA
21770
Tarehe ya kuingizwa: 2012/05/20
Summary Maswali
kwa nini Uislamu unaamuru kuwanyonga wanaoritadi? Je hilo haliendani kinyume na uhuru wa kila mmoja kuabudu anacho kitaka?
SWALI
kwa nini Uislamu unaamuru kuwanyonga wanaoritadi? Je hilo haliendani kinyume na uhuru wa kila mmoja kuabudu anacho kitaka?
MUKHTASARI WA JAWABU

Kuritadi ni kitendo cha wazi kabisa cha kutoka katika dini, na mara nyigi tendo hilo hutumika kama ni nyenzo ya kuwadhoofisha wengine kiimani na kuwafanya waache dini yao, na hatimae kuwatoa na kuwaweka nje ya dini. Wanaohukumiwa hukumu ya kuritadi, ni wale wanaolidhihirisha tendo hilo kwa wengine, ama wale walioritadi kifichoni bila ya kuidhihirisha imani yao kwa wengine, hao hawahusiki na hukumu hiyo. Lililo sawa ni kamba, adhabu inayotolewa kwa watu hao inahusiana na kosa la kijamii la kuwapoteza wengine, na si kwa sababu ya imani zao binafsi zilizo potofu.

Mwenye kuritadi huivunja mioyo ya Waumini waliomo ndani ya jamii, na husababisha imani za watu dhaifu au walio wachanga kiimani kupwaya. Wakati ambapo Uislamu ulipokuwa bado ni mchanga, kulikuwa kuna maadui wa Uislamu ambao kazi yao ilikuwa ni kujifanya kuwa wao ni Waislamu, kisha baadae huritadi na kuukanusha Uislamu, hufanya hivyo ili kuizorotesha dini pamoja na kuwazorotesha Waislamu kiimani.[i]

 

Uislamu ukiwemo katika njia za kujidhatiti na kujiimarisha, ulitangaza sheria kali juu ya watu wanao ritadi, na kwa upande mwengine, Uislamu uliweka sharti nzito katika kuithibitisha imani hiyo ya kuritadi kwa mtu fulani, ili kuepukana na kule kuhukumiana kiholela, ndiyo maana katika tarehe kukawa hakukuonekana kuwepo wengi waliyo hukumiwa kwa ajili ya kuritadi. Hilo ndilo lililoifanya hukumu hii kutokuwa ni tishio la kuwaathiri watu Kisaikolojia, kiasi ya kwamba hakukutokea mtu aliyehisi kuwa maisha yake yako hatarini kwa ajili ya imani yake aliyonayo.

 


[i] Rejea Suratu Aal-Imraan Aya ya 72.

 

JAWABU KWA UFAFANUZI

Ili jawabu ifahamike vyema zaidi, tunatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo:

La kwanza: mritadi ni mtu gani? Mritadi ni mtu aliyetoka katika Uislamu na kuingia katika ukafiri.[1] Kutoka katika Uislamu kunakamilika kwa kuikanusha misingi ya dini au kuukanusha mmoja kati ya misingi hiyo kama vile kuukanusha upweke wa Alla (s.w), utume au siku ya malipo, na yawezekana mtu kuritadi kwa kukanusha moja kati ya mambo ya wajibu yanayokubaliwa na Waislamu wote, iwapo kulikanusha jambo hilo kutapelekea kuukanusha utume au uungu wa Mola Mtakatifu, huku akiwa yeye ni mwenye kuelewa na kuwa na akili timamu katika matendo yake ya ukanushaji huo.[2]

La pili ni kwamba: kuna aina mbili za waritadi:

1- Mritadi wa fitra (asili) yake ya mwanzo ((مرتد فطری, naye ni yule ambaye ilipotunga mimba yake, baba yake na mama yake walikuwa ni Waislamu, na baada ya kubaleghe akadhihirisha kuwa yeye ni Muislamu na baadae akaritadi.[3]

2- Mritadi wa mila (dini) ((مرتد ملی, naye ni yule  mtu ambaye ilipotunga mimba yake, wazazi wake walikuwa ni makafiri naye alipobaleghe akawa amedhihirisha ukafiri, na baadae akasilimu kisha akarudi tena katika ukafiri.[4]

La pili: hukumu ya mritadi katika dini tofauti na madhehebu mbali mbali.

Ndani ya madhehebu ya Kishia, mritadi huwa na aina mbali mbali za hukumu ndani ya kisheria, zikiwemo hukumu za kurithi, kuoa na mengineyo. Lakini swali lililoulizwa halihusiani na masuala haya.

Hukumu ya mritadi wa fitra (مرتد فطرى): iwapo mritadi huyo atakuwa ni mwanamme, kuhumu yake huwa ni kuuliwa, na hata kama atatubia mbele ya kadhi, toba yake huwa haikubaliwi. Na hukumu ya mritadi wa mila (مرتد ملّى) si kuuliwa, bali hutakiwa atubie. Iwapo yeye atatubia, huachiwa huru, na akikataa kutubu huuliwa. Lakini mritadi wa kike kaitka aina zote mbili huwa hauliwi, bali hushauriwa kutubia na akikataa hubakishwa jela hadi akubali kutubia.[5]

Ama katika madhehebu ya Kisunni, kwa mtazamo wa maulamaa walio wengi ni kwamba: mritadi wa aina yeyote ile huwa anashauriwa kutubia, endapo atakubali kutubia huwa anaachiwa huru, na endapo atakataa huwa anauliwa bila kutofautisha baina ya mwanamke na mwanamme au mritadi wa fitra na wa mila.[6]

Hukumu ya mwenye kuritadi katika dini nyengine za Mungu zilizotangulia ni kuuwawa.[7]

Hivyo basi hapa tunaweza kusema kuwa: mitazamo ya dini zote pamoja na madhehebu yake mbali mbali hulihesabu kosa la kuritadi kuwa ni kosa linalostahiki adhabu ya kifo, ingawaje kwa namna moja au nyengine huwa kunazingatiwa mambo na masharti maalumu katika utekelezaji wa hukumu hiyo.[8]

La tatu: ili ieleweke vizuri falsafa ya kuadhibiwa mwenye kuritadi, tunatakiwa kuzingatia nukta zifuatazo:

1- Hukumu za Kiislamu zimegawika sehemu mbili, nazo ni hukumu za jamii kiujumla na hukumu za mtu mmoja mmoja. Hukumu za kijamii zimepangwa ili kuyalinda maslahi ya jamii kiujumla, na baadhi ya wakati hukumu hizi huwa zinaweza kuifinya mipaka ya uhuru wa mtu fulani kwa ajili ya kufidia maslahi ya jamii, na hakuna jamii inayoweza kulikanusha jambo hili.

2- iwapo mritadi atakuwa ametumia jitihada zake zote katika kuifahamu haki na ukweli, huyo atakuwa ni mwenye msamaha mbele ya Mola wake, na katka matendo yake binafsi hatohisabika kuwa ni muovu au mpotoshaji,[9] lakini iwapo mtu atafanya uzembe katika kuitambua haki na ukweli, huyo atahesabiwa kuwa ni mkosa katika matendo yake binafsi endapo matendo hayo hayatoidhuru jamii. Wakati wowote ule mritadi atapoidhihirisha imani yake na kuitandaza mbele ya jamii, hapo basi tendo lake hilo alitoacha kufuatiliwa na sheria za kijamii zilizopangwa na Mola Mtakatifu, kwani tendo hilo litakuwa tayari limeshaikiuka mipaka yake yeye binafsi na kusambaa nadani ya jamii, na hapo ndipo atapokabiliwa na sheria na kuhesabika kuwa ni mkosa kijamii. Na dalili hasa ya yeye kukabiwa na sheria hizo ni kwamba:

La kwanza: yeye amezivuruga haki za wengine, kwa kule kuzitia ushawishi na wasiwasi akili za wanajamii, na ni kitu kilicho wazi kuwa: kuwachafuwa watu akili zao na kuziparaganya kwa kutumia udhaifu iliopo ndani ya jamii, ili kuwapotosha na kuzidhoofisha imani zao, huhesabiwa kuwa ni kosa lisilosameheka kiholela. Na wanajii wote wanafahamu kuwa: wao hawana wadhifa wa kusimamisha midahalo kwa ajili ya kuitetea dini na imani yao, bali kazi hiyo inatakiwa kushughulikiwa na wataalamu wa kidini, kwa hiyo mritadi anatakiwa kukabiliana na waatamu hao kwa kupatiwa tiba ya maradhi yake, na sio kuyaeneza maradhi hayo ndani ya jamii.

La pili: tukifumbia macho suala la kuwa: kuihifadhi na kuiweka salama imani ya wanajamii ni haki ya kila mmoja inayostahiki kulindwa na sheria, kwa upande mwengine Uislamu unaamini kuwa: kubakia salama imani ya jamii ni maslahi yasiyoweza kufumbiwa macho na sheria, na hilo ndilo lililoifanya dini ya Kiislamu kuwataka waumini wake kuzitukuza aina zote za utajo wa dini yao.[10] Na kwa upande wa pili ikakataza uvurugaji wa maliganio ya dini na utajo wake.[11]

Natija ya yote hayo yaliopi ni kwamba: yawezekana kuritadi ikawa si kosa kibinafsi, lakini kijamii huhesabiwa kuwa ni kosa.

3- Kwa kuzingatia uzito wa kosa la kuritadi, falsafa ya kuhukumiwa mritadi inaweza kuelezewa katika vipengele vifuatavyo:

 

A: Hukumu na ulazima wa kuhukumiwa mritadi

Hukumu inayomkabili mritadi, ni kifungu maalumu cha sheria kinachomkabili mwenye kuritadi kwa kosa la uvurugaji wa nidhamu ya jamii, na hukumu yake huwa inatofautiana kutoka hatua moja hadi nyengine kwa jinsi ya uzito na kiwango cha uvurugaji huo kilivyo. Kwa hiyo iwapo mtu ataichafua jamii kitabia na kiimani katika hali maalumu, sheria nayo itatakiwa kumkabili yeye kwa jinsi ya uzito wa machafuzi aliyoyasababisha ndani ya jamii. Ingawaje jamii yawezekana ikawa na maendeleo ya Kiteknolojia ya hali ya juu kabisa, lakini bado jamii hiyo haitoweza kufaulu na kuyafikia malengo halisi ya uanaadamu bila ya kuwa na dini iliyosalimika kiakida (kiimani). Hivyo basi dhambi yeyote ile itakayosababisha mmomonyoko wa imani ndani ya jamii, dhambi hiyo huhesabiwa kuwa ni dhambi hatari inayostahiki kuhukumiwa kisheria, na mfano wa dhambi hiyo ni kama vile kumtukana Mtume wa Mola Mtakatifu au Maimamu watakatifu, kwani kufanya hivyo kutapelekea udhoofishaji wa dini na imani ndani ya jamii na hatimae kuibomoa dini ya Mola Mtakatifu.

 

B: sheria huwa ni kizuizi kinachoizuia dhambi ya kuritadi kuenea ndani ya jamii

 

Mritadi asipoidhihirisha imani yake ya kuritadi, hatoweza kuidhuru jamii, na kinachoweza kumfanya yeye aidhibiti imani yake na kutoisambaza, ni kule kuikhofu  na kuiogopa sheria kali inayowakabili wenye kuritadi.

C: kuifahamisha jamii umuhimu wa dini ya jamii

Kila mpangaji wa sheria huwa anazipanga sheria zake katika mfumo na mtindo maalumu wenye kuonyesha ndani yake uzito wa masuala na haki mbali mbali za jamii. Kuitangaza sheria kali dhidi ya wenye kuritadi, huwa kunaonesha umuhimu wa kuihifadhi na kuilinda dini na imani ya wanajamii.

D: Adhabu ya kuritadi ni msukumo maalumu unaoweza kuwafanya watu kutafakari kwa upana zaidi kabla ya kuingia ndani ya Uislamu

Kumuadhibu anayeritadi huwa ni changa moto kwa kila asiyekuwa Muuslamu kuutafakari Uislamu na kuusoma vizuri zaidi kabla ya kuingia ndani yake, jambo ambalo huwa ni silaha bora dhidi ya kuzaliwa imani dhaifu ndani ya jamii ya Kiislmu.

E: kupata afueni ya adhabu ya Akhera

Mtazamo wa dini unaonesha kuwa adhabu ya dunia huwa ni sababu ya kumpunguzia aliyehukumiwa kwa adhabu hiyo na kupewa afueni ya adhabu ya Kiama. Mola ni mwenye huruma ya hali ya juu, na kumumuadhibu mja mara mbili (Duniani na Akhera) ni kinyume na huruma ya Mola wetu. Katika dini yetu kuna maandiko yanayoonesha kuwa Waislamu wa mwanzo walikuwa wakiamini hivyo, na walikuwa wakiwashawishi watenda makoso kuyakubali na kukiri makosa yao, ili waikubali adhabu ya Duniani kwa ajili ya kuiepuka  au kupata afueni ya adhabu ya Akhera.

Zingatio: ingawaje adhabu ya Duniani huwa ni sababu ya kupata afueni siku ya Kiama, lakini kuna njia nyengine ya kumsaidia mfanya makosa kuiepuka adhabu ya Akhera, nayo ni kutubia toba ya kweli isio na doa ndani ya ukweli wake. Iwapo mfanya kosa atatubia toba hiyo bila ya kuwa na haja ya kuhukumiwa na mahakama ya kisheria ya ndani ya maisha ya kidunia, huyo atakuwa ni mwenye kupata msamaha wa kosa lake.

4- Kuwa na hadhari katika utekelezaji wa sheria; kuna mengi  yaliotajwa katika falsafa ya kumhukumu mritadi pamoja na Aya za Qur-ani, lakini yawezekana kuwa falsafa na hukumu za Aya hizo zimeshuka kwa kutokana na zile fitna za Mayahudi waliokuwa na njama za kuutokomeza Uislamu,[12] kwa hiyo hukumu hizi zitakuwa hazimhusu kila mritadi. Kwa upande wa pili tataona kuwa; kuna baadhi ya waritadi wasiokuwa na malengo ya kuupotosha uma, na wala kuritadi kwao hakuleti madhara yeyote yale ndani ya jamii ya Kislamu, lakini bado sheria inayomkabili huwa ni ile ile bila ya kuwa na mabadiliko baina yake na yule mritadi mharibifu. Ni sababu gani basi ya yeye kutopata afueni katika adhabu hiyo? Kwa ibara nyengine ni kwamba; iwapo falsafa ya kuadhibiwa mritadi ni kule kuichafua jamii na kuzitingisha imani za watu, mritadi huyu basi haonekani kuwa na kosa hilo!

Jawabu: mara nyingi muwekaji kanuni au sheria, huwa anaziweka sheria hizo kwa kutokana na aina ya matendo au makosa yalivyo, na wala yeye hawaangalii watendaji ni watu wa aina gani, hata kama falsafa ya kuwekwa hukumu hiyo itakuwa haionekani katika kila kitendo cha mtendaji wa aina hiyo ya matendo, na hilo ndilo linaloitwa ‘uchukuaji wa hadhari katika upangaji wa sheria’. Jawabu tulioitoa hapa tukizungumzia namna ya upangaji wa sheria, inaweza kufahamika vizuri iwapo tutazingatia vipengele vifuatavyo:

A: mara nyingi mpangaji wa sheria huwa hawezi kumpa mtu uhuru wa kuitumia sheria fulani, katika hali tu ya kuwepo kwa sababu zilizosababisha kupangwa sheria hiyo. Kwa mfano: sababu halisi ya kuwekwa sheria ya kutoegeza gari pembezoni mwa barabara, ni kuondoa ongezeko la msongomano wa magari barabarani, hali ya kuwa msongomano huo waweza ukawa unatokea katika baadhi ya wakati tu na sio wakati wote, lakini sheria za usalama wa barabarani huwa ni zenye kufanya kazi katika hali zote mbili, bila ya kuweka tofauti ya aina fulani katika kumhukumu muegeshaji wa gari katika eneo hilo. Hii ni kwa sababu ya kutokuwepo uwezekano wa kuiwacha sheria ndani ya mikono ya jamii kiholela, kwani jambo hilo laweza kuhatarisha amani ya jamii hiyo.

B: Mara nyengine huwa kuna hukumu zenye umuhimu wa hali ya juu na kwa kutokana na umuhimu huo, mpangaji wa sheria huwa analazimika kuwa na uangalifu pamoja na hadhari katika kuilinda sheria hiyo, na hilo ndilo linalosababisha kuifanya hukumu hiyo kumgusa kila mtendaji atakaye kwenda kinyume na sheria hiyo, na kutolifumbia macho tendo hilo katika hali yeyote ile ya utendaji wa tendo hilo.

Kwa mfano: silaha za kijeshi huwa zinatakiwa kuwa mbali na majengo ya raia, kwa ajili ya usalama wa raia pamoja na usalama wa silaha hizo, kwa hiyo kila silaha hizo zikiwa mbali zaidi na raia usalama nao huwa ni wa hali ya juu zaidi. Hilo ndilo linalowafanya wahusika wa usalama kuyarefusha masafa yaliopo baina ya raia na maeneo ya kijeshi ili kuwa na yakini na usalama wa raia.

Uislamu nao pia huwa unalizingatia suala hilo, na ndio sababu hasa zilizoufanya Uislamu kuzitanua baadhi ya sheria zake na kutozingatia sababu za mtu mmoja mmoja katika utendaji wa aina fulani ya makosa yanayoweza kuhatarisha usalama wa imani ya jamii.

Kwa ajili kupata ufafanuzi zaidi juu ya falsafa ya upangaji wa sheria au falsafa ya hukumu za kisheria ndani ya Uislamu rudia vitabu vifuatavyo:

Falsafa ya sheria, cha Qudrati Llahi Khosro-Shaahi na Mustafa Daanesh-Pazuu, uk: 201-222; vile vile Adlu Ilahi cha Shaiid Mutahhari; pamoja na Tafsiri Almiizaan Aya

"لا اكراه فى الدين" juz: 2, uk: 278 au Tafsiri Nemune, juz: 2, uk: 360.

 

 


[1] Kitabu tahriirul-wasiila cha imamu Khomeiny juzuu ya pili ukurasa wa 366 na Al-mughni cha Ibnu Qudama juzuu ya kumi ukurasa wa 74.

[2] Rejea kitabu kilichopita juzuu ya kwanza ukurasa wa 118.

[3] Kitabu hicho hicho juzuu ya pili ukurasa wa 366.

[4] Imamu Khomeini/tahriirul-wasiila juz: 2/ uk: 336.

[5] Kitabu kilichopita juz:2 uku: 494

[6] Kitabu al-fiqhi alaa madhaahibul- arba-a cha Abdul-Rahmaan Al-Jazaair juz:5 uk: 424. Abu Hanifa naye ni kama Mashia anatofautisha baina ya mwana mke na mwanamme. Rejea badaai-u sanaai-i cha Abuu Bakar Al-Kasaai juz:7 uk:135. Hassan Al-Basri hakubaliani na wito wa kutubia kwa aliye ritadi. Rejea kitabu al-mughni cha Ibnu Qudaama uk: 76 juz: 10.

[7] Rejea Agano jipya sifr tauria mlango wa 13 uk: 80 - 357 ambayo ni tarjuma ya Kifarsi ya William Gelen iliochapishwa na King's House London mwaka 1856. Vile vile sifr thania al-ishtira-a mlango wa 13 ku: 80 – 379 chapa ya Beirut Aarul-Mashriq, pia uk: 06- 305 wa tarjuma ya Agano jipya ya mwaka 1357 shamsia iliotolewa na kitengo cha kufaasiri na kutarjumu Biblia kilichoko Tehran.

[8] Lakini kuna maulamaa ambao wanao ona kuwa hukumu ya mritadi ni kuonywa kwa kupewa adabu maalum, na mwenye kuainisha aina hiyo ya maonyo ni kiongozi wa kidini, na Uislamu haukuzungumzia juu ya ufafanuzi wa aina ya maonyo hayo. Kwa hatuwezi kutoa kauli ya moja kwa moja kuwa hukumu ya kuritadi ni kifo. Rejea uk: 387 wa juz: 3 wa kitabu diraasaat fii wilayatil-faqiih wa fiqhi daulatil- Islaamiyya cha Hussein Ali Muntadhari, vile vile irtidaad dar Islam uk: 129 hadi 148 cha Isa Wilaayatiy.

[9] Mola katika Qurani anasema: (Mola haikalifishi kutenda isicho kimudu) Aya 286 ya Suratul-Baqara.

[10] Rejea Suratul- Hajji Aya ya 32.

[11] Rejea Suratul- Maaida Aya ya 2.

[12] Suratu Aalu Imraan Aya ya 72.

 

 

TARJAMA YA JAWABU KATIKA LUGHA NYENGINE
MAONI
Idadi ya maoni 0
Tafadhali ingiza thamani
mfano : Yourname@YourDomane.ext
Tafadhali ingiza thamani
<< Niburute.
Tafadhali ingiza kiasi sahihi ya usalama Kanuni

MPANGILIO WA KIMAUDHUI

MASWALI KIHOLELA

YALIYOSOMWA ZAIDI