Please Wait
13040
Hadhithi Kisaa (Hadithi ya joho) ambayo imenukuliwa ndani ya kitabu cha Sheikh Abbas Qummiy kijulikanacho kwa jina la Mafaatiihul-jinaan, ni Hadithi iliyobeba ndani yake ujumbe mzito wenye umuhimu wa aina mbili. Umuhimu wa kwanza ni kule Hadithi kuwa na fungamano la moja kwa moja na suala la uimamu na uongozi, na umuhimu wa pili ni kule Hadithi hii kufungamana moja kwa moja na utakaso maalumu waliokuwa nao maimamu waongofu.
Uwalii, uimamu na uongozi wa Ahlul-Bait (a.s) ni jambo lililotolewa ushahidi kamili kupita Hadithi takatifu za Mtume (s.a.w.w). Mtume (s.a.w.w) alitumia nyenzo mbali mbali ili kuwafahamisha watu kuhusiana na uongozi wa Ahlul-Bait (a.s) baada yake, uongozi na ukhalifa ambao ni maalumu kwa watu hao na sio haki kwa mtu mwengine kushika nafasi hiyo. Kule Yeye (s.a.w.w) kuwakusanya na kuwafinika Ahlul-Bait kwa joho lake (kisaa) kwenye nyumba ambayo hawakuwepo watu wengine isipokuwa wao tu, ni tendo maalumu lenye nia ya kutoa stakabadhi na ithibati juu ya madaraka waliyonayo Ahlul-Bait (a.s) katika kushika nafasi ya ukhalifa baada ya Mtume (s.a.w.w), pia ndani ya Hadithi kisaa kuna ibara maalumu alizozitumia Mtume (s.a.w.w) zenye kulenga ile haki aliyonayo Ali (a.s) katika nafasi ya ukhalifa ambao yeye (Ali) (a.s), alitakiwa kuishika baada ya Mtume (s.a.w.w) kufariki, maneno yaliyotumika ndani ya Hadithi kisaa, ni yenye kuonesha fungamano madhubuti lililopo baina ya Mtume (s.a.w.w) na Ahlul-Bait (a.s).
Wengi miongoni mwa wanazuoni wameitumia ibara isemayo:
" واَذْهِبْ عَنْهُمُ الرِّجْسَ وَ طَهِّرْهُمْ تَطْهيراً"
ilioko ndani ya Hadithi kisaa katika kusimamisha dalili juu ya suala la utakaso walionao Maimamu (a.s). hivyo basi hadithi hii ni yenye umuhimu mkubwa katika kuithibitisha haki ya ukhalifa pamoja na utakaso wa Ahlul-Bait (a.s).
Kuna mlolongo mkubwa wa Hadithi zilizoizungumzia Hadithi ya kisaa, ingawaje baadhi yake ziliigusia Hadithi hiyo kimukhtasari tu, lakini ni jambo tosha linye kuitia nguvu Hadithi hiyo.[1] Hadithi hizo mbali mbali zimeashiria na kuelezea kuwa: Mtume (s.a.w.w) aliwakusanya watu wa nyumba yake ambao ni: Ali, Fatima, Hasan na Husein (a.s), kisha akawafunika kupitia joho lake huku Naye (s.a.w.w) akiwa pamoja nao, kisha akatamka ibara ifuatayo:
إِنَّما يُرِيدُ اللَّهُ لِيُذْهِبَ عَنْكُمُ الرِّجْسَ))
Maana yake ni kwamba: “Kwa hakika Mola Ametoa ahadi ya kukuondoleeni uchafu (kukutakaseni)”
Hadithi hii haikupokewa tu na wapokezi wa Hadithi wa madhehebu ya Kishia, bali kuna wengi miongoni mwa wanazuoni wa Kisunni walioipokea na kuinukuu Riwaya hiyo kutoka kwa watu tofauti, miongoni mwa wanazuoni hao ni Haakim Haskaaniy Niishaabuuriy ambaye ameinukuu Hadithi hiyo kutoka kwa watu mbali mbali, na mwenngine aliyeipokea Hadithi hiyo kutoka kwa watu mbali mbali, ni Sayyid Ibnu Taawuus.[2]
Ingawaje Riwaya hii imezunguziwa na kunukuliwa na vitabu mbali mbali, lakini sisi katika uhakiki wetu wa Riwaya hii tutayangalia tu yale mapokezi na nukuu za Riwaya hii yaliyonukuliwa na Sheikh Abbas Qummiy ndani ya kitabu chake Mafaatihul-jinaan.
Kwa mtazamo wetu sisi nukuu zilizoinkuu Riwaya hii ambazo zimetajwa ndani ya kitabu cha Sheikh Abbas Qummiy, ni zenye nia na malengo ya kuyaashiria masuala mawili muhimu, nayo ni:
1- Kutoa stakabadhi na ithibati kuhusiana na suala la uimamu na uongozi wa Maimamu watakatifu (a.s):
Kwanza kabisa aple tutapoiangalia Hadithi hii, tutaikutia kuwa ina nia ya kutoa bishara na uthibitisho wa ile haki maalumu ya uongozi na mamlaka ya ukhalifa yenye kuwahusu tu watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w), haki ambayo haimstahikii mwengine yoyote yule zaidi Yao (a.s), na jambo limeonekana kwa zaidi ya mara moja kutiliwa mkazo na Mtume Mwenyewe (s.a.w.w). kuna vipengele tofauti vinaonekana kuhusika na suala hilo, na baadhi vipengele hivyo ni kama ifuatavyo:
A- Nafasi ya Ahlul-Bait (a.s) katika uongozi: mara kwa mara ndani ya zama na nyakati tofauti Mtume (s.a.w.w) alionekana kuutangaza unaibu wa Ali (a.s) wa kuishika nafasi ya ukhalifa baada Yake (s.a.w.w). Na Hadithi kisaa ni moja tu ya ushahidi kuhusiana na suala hilo, si mara moja wa mbili alizoonekana mtume kumtangaza Ali (a.s) kuwa ndiye msika bendera, ndugu yake na ndiye khalifa au naibu wa kuishika nafasi ya uongozi baada Yake (s.a.w.w).[3] Na ili Mtume (s.a.w.w) azidi kuwazindua watu na kuwafahamisha umuhimu wa Ahlul-Bait pamoja kuilinda heshima yao mbele ya watu wakati wa uhai wake na baada ya kufa kwake, Yeye (s.a.w.w) alionekana ndani ya Hadithi kisaa kutoa sisitizo zito kwa ajili hilo kwa kusema:”Hawa ndio Ahlu-Bait wangu (kizazi changu) na ndio wanaohusika zaidi na mimi, damu yao ndiyo damu yangu na nyama yao ndiyo nyama yangu, mimi huudhiwa na yale yanayowaudhi wao, na yanisikitisha yale yawasikitishayo, mimi nitamsimamishia vita kila yule atakayewasimamishia vita watu hawa. Mimi ninatokana na hawa (Ahlul-Bait) (a.s) na Hawa wanatokana na mimi, basi ewe Mola wangu shusha baraka, amani, upendo na usamehevu juu yangu mimi na wao pia, kwa kweli mimi nitampa mkono wa amani yule atakayewapa mkono wa amani Ahlu-Bait wangu na nitakabiliana na yule atakayekabiliana nao, pia mimi ninampenda yule awapendao na ninamchukia yule awachukiao.
B- Kuuhusisha uimamu na uongozi kwa watu wa nyumba Yake (s.a.w.w) peke yao:
Pale Imamu Hasan, Imamu Husein, Imamu Ali pamoja na Fatima (a.s) walipoingia kwa Mtume (s.a.w.w), Mtume (s.a.w.w) aliwafinika kwa joho lake (kisaa), kisha akamuomba Mola wake kuwatakasa kutokana na uchafu wa madhambi, kisha Aya isemayo:
إِنَّما يُرِيدُ اللَّهُ لِيُذْهِبَ...))
Yaani: “Kwa hakika na yakini Mola wako ameweka ahadi ya kukutakaseni nyinyi Ahlul-Bait kutokana na uchafu…”
Swali muhimu hapa ambalo tunataka kuwauliza watu, ni kuwa je hivi kitendo cha Mtume (s.a.w.w) kilikuwa kikiashiria maana na jambo maalumu au kilikuwa ni kitendo kisichokua na malengo yoyote? Moja kwa moja jawabu ya kila mmoja wetu itakuwa ni kusema kuwa: tendo hilo lilikuwa na malengo maalumu, kwani si jambo lenye kukubalika kuwa Mtume (s.a.w.w) juu ya cheo chote alichonacho awe anatenda matendo bila ya kujali malengo maalumu katika utendaji wake.[4] Ni maengo gani basi ambao Mtume (s.a.w.w) alikua akiyakusudia katika Hadithi kisaa?
Baada ya kila mmoja wetu kuisoma Aya hii, huku akiihakiki kisawa sawa, atagundua kuwa iwapo Mtume (s.a.w.w) asengeifunga Aya hiyo kwa kule kuwafunika watu wa nyumba yake (Ahlul-Bait) kwa joho lake, huku akikataa kumuingiza mtu mwengine ndani ya joho hilo, basi bila shaka kungelitokea baadhi ya watu ambao wangeliweza kuda kuwa nao ni miongoni mwa Ahlul-Bait (a.s), na ingelikuwa ni jambo rahisi kwa wake wa Mtume (s.a.w.w) kudai kuwa wao ni watu waliokaribu na Mtume (s.a.w.w) nao basi ni miongoni mwa Ahlul-Bait (a.s), hapo basi nao pia wangelihisabika kuwa ni wahusika kamili wa Aya hiyo. Ili Mtume (s.a) awaondolee shaka wafuasi wake, yeye alionekana katika baadhi ya Hadithi zenye kukizungumzia kisa cha tokeo hilo, kuiripiti mara tatu kauli isemayo: “Ewe Mola hawa ndio watu wa nyumba yangu, kwa hiyo watakase na uwaweke mbali na uchafu”.[5]
Pia ndani ya vitabu vya wanazuoni wa Kisunni imeelezwa kuwa: kwa muda wa kipindi cha siku arubaini Mtume (s.a.w.w) alikuwa akiwadaukia Ali na Fatima (a.s), huku akiwasalimia kwa kusema: “Amani rehema na baraka za Mola ziwe juu yenu enyi Ahlul-Bait, wakati wa sala umeshaingia Mola akurehemuni…”[6]
2-Thibitisho la utakatifu na utakaso wa Ahlul-bait:
Suala la pili muhimu lilizingatiwa na kuthibitishwa ndani ya Riwaya hii, ni utakaso walioupata Ahlul-Bait na hatimae utakaso huo kuwafikia Maimamu watakatifu (a.s). Hadithi ya kisaa ni kifafanuzi kamili cha aya iliyosema:
«إِنَّما يُرِيدُ اللَّهُ لِيُذْهِبَ عَنْكُمُ الرِّجْسَ»
Kwa hiyo kila kimoja miongoni mwa Riwaya na Aya ya Qur-ani ni vyenye kusaidiana katika kuufafanua utakaso wa Ahlul-Bait pamoja na Maimamu (a.s), kwani lengo la vieili hivyo ni kuufafanua uhakika huo na kuuweka wazi mbele ya wanaadamu.
Baadhi ya wanazuoni wa fani ya Tafsiri, wamelifasiri neno (الرِّجْسَ) kwa maana ya (shirki) au (dhambi kuu) kama vile zinaa na mfano wake, hali ya kuwa hakuna dalili yoyote ile yenye kulifunga neno hilo kwenye maana hiyo tu, bali neno hilo ni lenye kubeba ndani yake aina zote za uchafu (dhambi), kwani dhambi zote ni chafu wala hakuna dhambi iliyo safi, ndiyo maana Qur-ani ikavihesabu vitu kama vile: ushirikina, ulevi, kamari na unafiki kuwa ni miongoni mwa uchafu, na Qur-ani ililitumia neno (الرِّجْسَ) katika kuwafafanulia waja uharamu na ubaya wa vitu hivyo.[7]
Jengine la kuzingatia ni kuwa, matakwa na ahadi ya Mola si yenye kurudi nyuma. Aya:
«إِنَّما يُرِيدُ اللَّهُ لِيُذْهِبَ عَنْكُمُ الرِّجْسَ»
Ni dalili tosha ya kuwa Yeye (s.w) alitaka kuwatakasa bila ya kurudi nyuma, kwani neno: (إِنَّما) lina maana ya: “Kwa hakika na yakini, ni ahadi ya moja kwa moja kutoka kwa Mola” kwa hiyo ni jambo la wazi kuwa Mola si kuwa tu alitamani wao wawe ni watakatifu, bali Yeye (s.w) alitoa kauli na ahadi ya moja kwa moja ya kutaka kuwatakasa, Naye akaitimiza ahadi yake, kwani Mola si mwenye kurudi nyuma katika kuzitimiza ahadi zake. kwa hiyo kauli na ahadi ya Mola aliyowapa Ahlul-Bait aliitekeleza kwa kuwatakasa Woa (a.s) kutokana na uchafu. Pia elewa kua matakwa ya Mola yamegawika katika makundi mawili:
A- Matakwa yaliyobeba amri za kuwataka watu wawe na sifa au matendo ya aina fulani.
Amri za matakwa haya huwa zinawakabili waja wote kwa ujumla, huku kila mmoja akiwa na hiari ya kutenda au kuto tenda. Na hiyo ndiyo maana ya kuadhibiwa wale waliokataa kutenda kwa kutokana na kuutumia vibaya uhuru wao.
B-Matakwa yenye maana ya ahadi au kutoa habari maalumu inayohusiana na utendaji wa Mola mwenyewe.
Aina hii ya matakwa huwa inaonesha namna ya uwezo wa Mola ulivyokuwa mkubwa katika kuvitawala na kuviendesha viumbe vyake (s.w), au hua ni aina fulani ya utoaji wa habari juu ya ahadi fulani, huku wakati mwengine ikwa na maana tu ya kuonesha na kufafanua jinsi yeye atendavyo pale inapojiri kutenda.
Neno (إِنَّما) katika Aya iliyopita linamaaasha ile aina ya ahadi ambayo Ameahidiwa kutendeka, na wala haina maana ya kuwataka Ahlul-Bait wajitakase. Ili kuufahamu ukweli huo, unaweza kurudia vitabu vya vya elimu ya Tafsiri vya Madhehebu mbali mbali, huku ukiwa ni hakimu mwenye kutumia akili yake kisawa sawa na sio kuelemea upande mmoja bila ya hoja madhubuti, au kuwahukumu wengine kabla ya kufanya uhakiki kamili kutoka pande tofauti.
Tunataraji kuwa uhakiki huu utakuwa ni wenye kuleta faida tosha au kuwa ni msaada kamili kwa wale wenye kupenda kuihakiki dini yao kisawa sawa na sio kufuata mambo kiholela. Mungu atupe Moyo wa ukunjufu wenye mwanga wa kuhakiki kisawa sawa. Aamin.
[1] Nahjul-haqqi–wa-kashfus-sidqi, cha Hasan bin Yusuf Hilliy, uk/228 hadi 229, chapa ya Darul-Hijra, Qum Iran, mwaka 1407 Hijiria. Pia angalia Jam-u baina Sihahi Sunna au Sahihu Abu Daud, Muwatta-a cha Maliik, na Sahihu Muslim.
[2] Shawahidu-tanzii-liqawaaidut-tafsiil, cha Haakim Haskaaniy, juz/2, uk/17, chapa ya Tehran ya kitengo cha uchapishaji cha Tab-u-wa-nashri. Attaraaifu-fi-ma’arifati-madhaahibut-tawaaifu, cha Sayyid Ibnu Taawuus, juz/1, uk/124 ya kitengo cha uhapishaji cha Nashru-Khayyaam ya mwaka 1400 Hijiria.
[3] Pale Ali (a.s) alipokwenda kwa Mtume (s.a.w.w) akamkuta Mtume (s.a.w.w) amejifinika joho kisaa, alimtolea salamu, na Mtume (s.a.w.w.) akamjibu kwa ibara ifuatayo:
قالَ لَهُ وَعَلَيْكَ السَّلامُ يا اَخى يا وَصِيّى وَخَليفَتى وَصاحِبَ لِواَّئى))
Maana yake ni kwamba: “Mtume (s.a.w.w) akamjibu: nawe amani iwe juu yako ewe ndugu yangu, ewe wasii wangu na naibu wangu na mshika bendera yangu”.
[4] Suratun-Najmu, Aya ya 3 hadi ya 4.
[5] Aamaalis-Saduuq, cha Sheikh Saduuq, chapa ya mwaka 1400 Hijiria ya kitengo cha uchapishaji cha Aa’lamiy Beirut Lebanon.
[6] Muujamul-ausat, cha Tabaraniy, juz/17, uk/438 .
[7] Surtul-Hajj, Aya ya 30. Mida, Aya ya 90, Tauba, Aya ya 125 na An’a’am, Aya ya 145.