Please Wait
8221
Katika tokeo muhimu la Karbala, kulikuwa kuna aina nyingi za nyuso zilizong’ara, na baadhi ya nyuso hizo zilikuwa ni nyuso za watoto wadogo, lakini Tarehe haikunukuu habari kamili kuhusiana na nyuso zote za watoto hao. Lakini mmoja miongononi mwa watoto waliotajwa na Tarehe, ni Ruqayya mwana wa Husein bin Ali (a.s), na jina Ruqayya linaonekana wazi kunukuliwa na vitabu vya Tarehe, ikielezewa kuwa yeye (a.s) alikuwa ni bint wa Imamu Husein (a.s). baadhi ya vitabu vya maombolezo ya Karbala, vimeonekana vikinukuu kauli ya Imamu Husein (a.s) iliyokuwa ikisema: “ewe dada yangu, ewe Ummu Kulthuum, nawe ewe Zainab, nawe ewe Ruqayya, nawe ewe Fatima nawe ewe Rubaab! Angalieni na muzingatie kwa makini kuwa, iwapo mimi nitauwawa, basi msije mkararua nguo zenu kwa hasira na huzuni, wala msije mkazipara nyuso zenu kwa huzuni, na wala msije kusema maneno yasiokuwa na maana kwa hasira na uchungu mtakao upata kutokana na kifo changu”[1]
Kwa jinsi ya ibara ya maneno ya Imamu Husein (a.s) ilivyo, haionyeshi ibara hiyo kuambiwa mtoto mwenye kiasi cha umri wa miaka mtatu au mine. Na katika vitabu vyengine kuna ibara kutoka kwa Imamu Huein (a.s), zisemazo: “ee Zainab we, nawe ewe Sukaina ee mwanangu we, ni nani atakayebakia nanyi baada yangu?, Nanyi ewe Ruqayya na Ummu-Kulthuum, nyinyi ni amana ya Mola ilioko kwangu mimi, leo basi ahadi yangu imeshakaribia”.[2]
Kwa mtindo wa ibara hii iliokuja hapo juu, haionekani kuwa ni ibara nzito kiasi ya kwamba iwe ni ibara isiyodirikiwa na mtoto mdogo wa miaka mitatu au minne, kwa hiyo yawezekana Imamu kuwa alikuwa akizungumza na wanawe pia akiwemo bint yake (Ruqayya) ambaye ni mtoto wa miaka mitatu au mine kupitia ibara hiyo, pale alipokuwa akimwita mtoto huyo (ewe Ruqayya…). Moja kati vitabu muhimu vya Tarehe vilivyomzungumzia bint huyu (a.s), ni kitabu (Kaamil Bahaai) cha Imadud-Diin Tabari. Ndani ya kitabu hicho imeelezwa kuwa: bint ya Husein alikuwa ni mwana wa miaka mitatu aliyekuwa akimpenda sana baba yake, na baada ya tokeo la Ashura alipokuwa usingizini, aliota kwa yeye ameka pembeni mwa baba yake, alipoamka alimtafuta baba yake, huku akisema: “nimeshachoka kustahamili ee baba uko wapi”, akaulizwa kwani umeona nini usingizini? Akajibu: “niliona kuwa nimekaa pembeni mwa baba yangu, huku akiwa yeye amenishikilia ubavuni kwake”. Yazidu alipopata habari kuhusiana na ndoto hiyo, aliwambia wafuasi wake: “nendeni mkamuoneshe kichwa cha baba yake.
Kisha wao wakaenda mbele ya Ruqayya na wakafunua sahani ilokuwa mikononi mwao, naye aliokiona kichwa cha baba yake akapiga ukenja na kufariki papo hapo”.[3] Lakini wanazuoni wengi ni wenye kuthibitisha kuwepo bint huyo aliyeishi baada ya vita vya Karbala, hii inatokana na kuwepo kwa vithibitisho vyenye kulithibitisha suala hilo. Mmoja kati ya waandishi aliyeandika kitabu (Shakhsiyyat Imamu Husein (a.s)), alikwenda kumuuliza mmoja kati ya wajuzi wa elimu ya Tarehe ambaye ni marehemu Aayatu-Llahi Mar-ashiy Najafiy kuhusiana na bint huyo, naye alijibu kwa kusema: “ingawaje sisi hatuna ushahidi wa tosha kuhusiana na kuwepo kwa bint huyo, lakini sisi hatuwezi kulikanusha sual la kuwepo kwake, kwani suala la kuwepo kwa bint huyo, limekuwa ni jambo mashuhuri”.[4] Jarida la (Zaair) linalofungamana na kitengo cha Imamu Ridha (a.s) kijulikanacho kwa jina (Astane Qudsi Radhawiy), toleo la namba 135 la mwaka 1384 Shamsia, limenukuu kisa kisemacho kuwa: Ayatu-Llahi Mirza Haashim Khurasaniy anasema: “mwanachuoni mkubwa sheikh Muhammad Ali Shaamiy aliyekuwa ni miongoni mwa watu wenye ikhlasi wa huko Najaf Iraq, aliniambia kuwa: babu wa mama yangu ambaye ni Sayyid Ibrahim Damashqiy aliyeishi zaidi ya miaka 90, ambaye nasabu yake inakwenda mpaka kwa Sayyid Murtadha, alikuwa na watoto watu wa kike tu. Usiku mmoja mtoto wake mkubwa wa kike alimuota Ruqayya (a.s) akimwambia: mwambie baba yako ampe habari Wali wa mji, kuwa kaburi langu limevamiwa na maji na linahitajia marekebisho. Alipoamka akampa habari baba yake, lakini baba yake akawa hakuchukua hatua yeyote kuhusiana na hilo, kwa kutokana na hali ya serikali ya zama zile ilivyo. Na ndoto hiyo ikamjia bint huyo kwa muda wa siku tatu mfululizo, huku baba akiwa halitilii maanani jambo hilo, hadi ilipofika siku ya nne, yeye mwenyewe akamuota Ruqayya (a.s) akiwa amekasirika huku akimwambia: kwa nini humpi habari Wali wa mji ili alifanyie matengenezo kaburi langu, yeye alipoamka alikwenda kwa kiongozi mhusika na kumpa habari kuhusiana na kisa cha ndoto ile. Wali akawakusanya wakuu wa madhehebu ya Sunni na Shia, yeye aliwataka waje siku ya pili huku wakiwa wamekoga na kujitoharisha ipaswavyo, ili waje kwa ajli ya kuifungua kufuli ilioko kwenye jengo la kaburi hilo. Na akatoa amri kuwa yeyote yule atakayeweza kuifungua kufuli hiyo, huyo ndiye atakayechukua jukumu la kulifukua kaburi na kumtoa maiti ili kaburi hilo lifanyiwe matengenezo, lakini hakuna aliyeweza kuifungua kufuli hiyo ila Sayyid Ibrahim. Walipolifukua wakaona kuwa maji yalikuwa yameingia kwenye kaburi hilo. Sayyid Ibrahim kwa muda wa siku tatu alikuwa akiupakata mwili huo huku akilia. Matengenezo ya kaburi hilo yalichukua muda wa siku tatu, lakini Sayyid Ibrahim alidumu katika eneo hilo bila ya kuhitajia maji wala chakula, na wala hakupitiwa lepe la usingizi. Na baada ya siku tatu kaburi likawa liko tayari, wakamrejesha maiti huyo ndani ya kaburi lake. Mnamo mwaka 1323 kaburi hilo lilifanyiwa marekebisho kupitia Haji Mirza Ali Asghar, aliyekuwa ni mshauri wa mfalme Sadru Aa’dham wa Iran, na tarehe 23 Rabiu-Thani 1405 likajengewa jengo jipya kupitia D. Muhammad Khatib, aliyekuwa waziri wa wakfu wa Syiria. Na ilipofikia mwaka 1419 mapambo yote ya kaburi hilo yakawa yameshakamilika. Mapambo yote ya jingo la kaburi hilo yalichukuliwa kutoka Iran na kupelekwa huko Syiria kwenye jengo hilo, na kazi ya kulipamba jingo hilo, ilifanywa na wahandisi wa Kiirani.
[1] Rejea kitabu (alluhuuf alaa qatli tufuuf) cha Abul-Qaasim Abul-Husein bin Sa’adud-Diin ibnu Taawuus, uk/141, chapa ya Uswa, Qum Iran, mwaka 1414 Hijiria, pia rejea A’alaamul-Waraa, uk/236.
[2] Mausua kalimaatil-Imam Husein (a.s), uk511, chapa kwanza ya mwaka 1373 Hijiria Shamsia ya Daarul-Maaruuf Qum Iran.
[3] Kaamil-Bahaai cha lmaadud-Diin Tabariy, juz/2, uk/179.
[4] Shakhsiyyat Husein, uk/615.