Please Wait
8065
Ruhusa ya kumfuata ulamaa maalumu katika matendo ya ibada za kila siku, inatakiwa kutolewa na akili ya mtu mwenyewe. Na wala ruhusa hiyo haingojewi kutoka kwa Maulamaa, huku kila mmoja akielewa umuhimu wa suala hili ndani ya maisha yake ya kila siku.
Katika hali yakawaida, mtu huwa ana sababu mbili zinanomfanya yeye kuwa ni mfuasi wa mtu maalumu:
1: Mwenendo wa kila mwenye akili huwa ni kuyatenda matendo yake kwa kupitia uoni wa kielimu aliokuwa nao, na pale anapohisi kuwa elimu yake ni changa kuhusiana na tendo analolitaka kulitenda, huwa anamuelekea mwerevu anayeutambua uhakika wa tendo hilo. Na mfano hilo ni kama vile mgonja kuenda kwa mtibabu ili amfafanulie ukweli wa magonjwa yake pamoja na kumpatia tiba ya magonjwa alionayo. Na hilo ndilo linalomfanya kila mwenye akili kumfuata ulamaa maalumu ili kupata ufafanuzi wa matendo na wadhifa wa kidini unaomuwajibikia yeye kisheria.
2: Kila muislamu anafahamu tosha kuwa dini yake ina maamrisho na makatazo maalmu yanayotakiwa kuzingatiwa na kila mfuasi wa dini hiyo, na ufahamu huu huwa ni dalili tosha itakayomfanya yeye kujihisi kuwa anawajibika kuyenda matendo yake kwa mujibu wa makatazo na maamrisho hayo yalivyo. Hapo ndipo anapojikuta kuwa; hana budi kufuata moja kati ya njia zifuatazo:
A: Awe na elimu ya kutosha itakayomuezesha kuyatambua maamrisho na makatazo hayo.
B: Awe na tahadhari katika matendo yake yote bila ya kufanya kosa katika uchaguzi wa matendo yake, yaani aliache kila lenye shaka na alishike kila lenye uhakika au kudhaniwa kuwa ni la sawa.
C: Awe ni mfuasi wa mwanachuoni maalumu, na matendo yake yawe yanaiegemea elimu na mitazamo ya mwanachuoni huyo katika matendo yake yote ndani ya maisha yake ya kila siku.
Mtu ataposhikamana na moja kati ya njia hizi tulizozitaja, atajihisi kuwa ameyatekeleza matakwa ya dini pamoja na wajibu wake ipaswavyo. Lakini njia ya mwazo huwa inahitajia muda mrefu ili yeye abobee kielimu, na kabla ya kuifikia daraja hiyo bila shaka atakuwa ni muhitaji wa moja kati ya njia mbili zilizobakia. Na njia ya pili nayo inahitajia mtu kuzielewa aina za haramu na halali pamoja na kuwa na elimu ya kutosha kuhusiana na hoja tofauti za wanazuoni mbali mbali kutokana na nyadhifa zinazomkabili, na hilo si jambo jepesi liwezalo kupatikana kirahisi au kufikiwa na kila mmoja. Njia pekee iliobakia ni njia ya tatu. Kwa ufafanuzi zaidi tunatakiwa kuelewa kwamba; dalili namba mbili iliopita hapo juu, inaonesha ulazima wa kumfuata mwanachoni katika masuala yote yanayodhaniwa kuwa ni wajibu au haramu pamoja na yale yanayodhaniwa kuwa ni sunna iwapo mtu atapendelea kuzitenda sunna hizo, lakini dalili namba moja inalithibitisha na kulizingatia suala la ufuasi katika aina zote za matendo. La muhimu kufahamu hapa ni kwamba suala la mtu kuweza kubakia kuwa ni mfuasi wa ulamaa wake baada ya kufa kwa mwanachuoni huyo, huwa linahitajia fatwa ya ulamaa huyo kuhusiana na suala hilo ndani ya uhai wake, iwapo yeye atakuwa hakutoa fatwa au haruhusu mtu kumfuata ulamaa wake baada ya kufariki kwake, hapo basi itambidi mtu mwenyewe ambaye ni mfuasi, kuwa na uangalifu juu ya suala hilo katika kuepukana nalo au kubakia kuwa ni mfuasi wa ulamaa wake.
Bado kuna dalili nyengine zinazohisiana na masuala ya ufuasi, lakini jukumu la kuzisimamisha dalili hizo litabakia mikononi mwa maulamaa, kwani wao ndio wajuzi zaidi wanaoutambua vyema uwanja huu.