advanced Search
KAGUA
11513
Tarehe ya kuingizwa: 2012/05/21
Summary Maswali
kwa nini Mola mtukufu hakuwahidi walimwengu wote na kuwafanya wawe ni watu wa kheri walioongoka?
SWALI
tunapoiangalia Aya isemayo: "وَلو شئنا لَأتينا كُلَّ نفس هُدها..." ambayo maana yake ni kwamba: “na kama tungelitaka, basi tungeliishikisha kila nafsi muongozo (uongofu) wake” hapa tutaelewa kuwa Mola hakutaka watu wote kuwa na uongofu. Na iwapo Mola angelikuwa amewatakia kheri viumbe wake wote, basi angeliwaongoza, lakini Yeye hakufanya hivyo. Basi ni nini dalili au sababu ya kutofanya hivyo?
MUKHTASARI WA JAWABU

Namna ilivyotumiwa Aya iliopita hapo juu ambayo ni (Aya ya 13 ya Suratu Sijda) katika usimamishaji wa dilili hiyo iliyosema kuwa: Mola hakuwaongoza viumbe wake, haikuwa sawa. Kwa sababu ni wazi kabisa kuwa; ukweli uko kinyume na usemi huo, kwani Mungu Mtukufu anamtakia kila mmoja kheri na mafanikio, na hilo ndilo lililomfanya kuwafanyia hisani waja wake, kwa kule kumpa kila mmoja akili ya kumuongoza. Ukirudia ndani ya Qur-ani utakuta kuna aina mbili za miongozo (hidaya), nazo ni:

A: muongozo wa kimaumbile.

B: muongozo wa kisheria.

Muongozo wa kimaumbile huwa ni wenye kufanya kazi ndani ya kila kitu, wala hakuna kitu kisichokuwa na aina hiyo ya muongozo. Muongozo huu ndio unaokilazimisha kila kitu kuwa na muelekeo maalumu wa kimaumbile hadi kuyafikia malengo yake yalioanishwa na Mola wake kuyafikia. Muongozo wa kisheria nao ni muongozo unaowahusu wenye nguvu za  kiakili tu zinazowawezesha kufikiria na kutatua mambo mbali mbali, na wala haumhusu yule asiyekuwa na nguvu hizo. Huu ni muongozo unaohusiana na mambo ya kisheria kama vile miongozo maalumu ya kusawazisha mja na kumungoza katika imani (akida) ilionyooka pamoja na kumuweka katika kanuni za Mola wake Mtukufu, zikifuatiliwa na makatazo au maamrisho maalumu. Muongozo huu huwa unawafikia wanaadamu kwa kupitia mitume au maimamu watakatifu (a.s). Kila mwanaadamu kwa namna moja au nyengine huwa ana himaya ya aina zote mbili za miongozo inayompa yeye msukumo wa kuufikia upeo wa malengo yake ya kibinaadamu.

Vile vile kuna Aya tofauti ndani ya Qur-ani zinazoonesha kuwa mwanaadamu ni kiumbe huru. Na moja miongoni mwa Aya hizo, ni ile Aya ya tatu ya Suratud-Dahr isemayo: “Hakika sisi tumemuongoza  njia mwanaadamu, naye yuko huru katika kushukuru (kushikamana nayo) au kukufuru (kuachana nayo)”. Mwanaadamu kuwa huru ndio maumbile yake alioumbiwa nayo, na suala la mwanaadamu kuwa huru ni suala la kimaumbila, na wala yeye hana mchango wowote ule kuhusu hilo, kwani suala la yeye kuwa na uhuru lilikuwa ni matakwa ya Mola wake na halikuwa ni chaguo lake binafsi.

Jenginge linaloweza kutoa msaada katika kufahamika jawabu ya suala lililoulizwa, ni kwamba: Mola Muumba hakuyafanya mambo tofauti ya ulimwenguni kutokea kiholela bila ya mpangilio maalumu, bali alilifanya kila jambo kufanyika na kutokea kwa kupitia sababu zake maalumu zinazoliwezesha na kulisukuma jambo hilo pamoja na kulielekeza katika ulimwengu wa matokeo. Muongozo wa Mola kwa mwanaadamu ndio sababu inayomfanya mwanaadamu kuuelewa ukweli, na kwa kupitia uhuru aliopewa huwa ana hiari ya kuuendea au kuto uendea ukweli huo, na bila ya kuwepo sababu hiyo muhimu, ingelikuwa ni vigumu kwake kuweza kuufikia ukweli huo. Kwa hiyo uhuru na akili ni nyezo toka kwa Mola wetu nazo ndizo sababu za mtu kuongoka au kutoongoka. Muongozo wa kimaumbile huwa umekivaa kila kitu akiwemo ndani yake mwanaadamu, lakini vile vile yeye amepewa nyongeza ya muongozo wa kisheria pamoja na uhuru wa kuchagua.

Kwa kutokana na kuwa mwanaadamu ni kiumbe huru, yeye basi anaweza kuufuata muongozo wa kisheria na kukifikia kilele cha uanaadamu wake, na kwa upande wa pili anaweza kuufunga mlango huo na kuufungua mlango wa muongozo wa kimaumbile ya kinyama alionayo, ambao hautofautiani sana baina yake na wanyama wengine, jambo ambalo litamfanya yeye kuzama katika sifa za unyama alizokuwa nazo, na hatimae kukifikia kilele cha unyama wake, na huo ndio upotofu. Hivyo basi tunachotakiwa kukielewa ni kuwa: Mola Muumba alikuwa ana uwezo wa kumuumba mwanaadamu katika hali ya maumbile maalumu yenye kumfanya yeye awe ni mtiifu bila ya kuwa na hiari katika utiifu wake, na huko ni kumyima yeye uhuru wake. Lakini Mola amemfanya yeye kuwa huru katika chaguo lake la kutii au kutotii na akampa muongozo wa kisheria pamoja na akili ya kutofautisha haki na batili. Na iwapo mtu atajitia kwenye kiza na upotofu, hapo basi nuru ya Mola wake itakuwa mbali naye. lakini iwapo yeye ataichagua haki na kutembea katika njia hiyo, hapo ndipo atapopata msaada wa nuru kutoka kwa Mola wake.

JAWABU KWA UFAFANUZI

kabla kulitafiti swala hili, kwanza kabisa inabidi kuzifafanua nukta zifuatazo:

1: Muumba Mtukufu katika Qur-ani anasema: “Na tungelitaka sisi kumuongoa kila mwanaadamu

(kwa kutumia nguvu bila ya kumpa uhuru wa kuchagua akitakacho) basi tungelimuongoa, lakini (kila mmoja yuko huru) na ndio maana ikawa (lakini) imeshathibiti kauli ya uhakika kutoka kwangu kwamba mimi kwa yakini nitaujaza moto wa Jahannam kwa kupitia watu na majini”.[1]

2: Maana ya hidaya (muongozo): hidaya au muongozo huwa una maana ya kumfanyia mtu hisani ya kumuongoza huku ukimtaakia kheri.

3: Aina za miongozo: ukiitafakari vizuri Qur-ani, utagundua kuwa kuna aina mbili za miongozo, nazo ni: muongozo wa kimaumbile na muongozo wa kisheria. Muongozo wa kimaumbile ni muongozo uliokidhibiti kila kitu, na kila kitu huwa kinaufuata muongozo huo kwa jinsi ya maumbile yake yalivyo, ili kukifikia kilele cha malengo ya kuumbwa kwake, huku muongozo huo ukikisukuma kitu hicho na kukielekeza katika kuyafikia malengo hayo. Mola Mtukufu anasema: “Akasema: Mola wetu ni Yule aliyekipa kila kitu umbile lake maalumu kisha akakipa muongozo wake[2] na katika Aya nyengine anasema: “Naye ndiye aliyeumba kisha akakiweka kila kitu mahala pake. Naye ndiye  aliyepanga makadirio ya (kila kitu) kisha kila kimoja akakipa muongozo wake[3].

Muongozo wa kisheria ni muongozo maalumu unaowahusu wenye akili tu, muongozo huu huwa unahusiana na utowaji maelekezo katika masuala kiimani na kisheria, pamoja na kumfahamisha mwanaadamu yale yanayopaswa kutendwa na yanayopaswa kuepukwa, hili ndilo linaloitwa: tabia njema. Muongozo huu huwa unawafikia wanaadamu kwa njia ya mitume au maimamu (a.s). Mola Mtukufu Anasema: “Kundi moja ameliongoa (Mola Mtukufu), na jengine likathibitikiwa na upotovu[4] vile vile akasema tena: “Na Mola humuongoza amtakaye (mwenye uchu (muelekeo) wa kuongoka)[5]. Tukiziangalia kwa makini Aya hizi, tutafahamu kuwa; muongozo uliokusudiwa ndani ya Aya hizi, ni muongozo wa kisheria, na muongozo huu unamuhusu kila mwanaadamu.

4: Uhuru wa mwanaadamu ambao ni wa kimaumbile: mwanaadamu ni mmilikiwa wa Mola Mtakatifu, naye ni kiumbe pekee (yeye pamoja na jini) miongoni mwa viumbe vya Mwenye ezi Mungu ailyeumbwa na kupewa uhuru, na kuna Aya chungu nzima zinazomuelezea na kutilia mkazo kuwa mwanaadamu ni kiumbe huru, kama vile Aya isemayo: “Na useme (utangaze) ukweli utokao kwa Mola wako, basi anayetaka kuukubali na aukubali, na anayetaka kuukanusha na akanushe”.[6] Na katika aya nyengine anasema: “Hakika sisi tumemuongoa mwanaadamu (kwa kumuonesha njia ya kheri na ya shari), naye yuko huru katika (kuifuata njia aitakayo) kushukuru au kukufuru”.[7] Bila shaka kila mmoja huwa anajihisi kuwa yuko huru pale atendapo matendo yake, basi kutenda au kutotenda huwa ni hiyari yake mwenyewe.

 

Chaguo lako la hili au lile ** ni alama ya uhuru ewe yule.[8]

 

Uhuru na hiyari ya mwanaadamu, ni sehemu ya maumbile yake isiokubali kutengana naye. Hapa utaona kuwa uhuru na hiyari ni mambo ya lazima na si ya hiyari, yaani mwanaadamu amelazimika kimaumbile kuwa na uhuru na wala hawezi kuepukana na uhuru huo. Na ingalikuwa mwanaadamu ameshauriwa kupewa au kutopewa uhuru, hapo basi angalikuwa na hiyari ya kuukubali au kuukataa uhuru huo. Lakini hadi leo hatujawahi kukutana na mtu asiyekuwa na uhuru wa kimaumbile. Hivyo basi mtu kuwa huru au kuto kuwa huru ni jambo lililoko nje ya uwezo wake. Dalili zote tulizozitoa zinathibitisha kuwa mwanaadamu ni kiumbe huru, na anatenda matendo yake kwa hiyari yake mwenye. Mwanaadamu kuwa huru inatokana na muongozo wa kimaumbile alioumbiwa nao. Kwa hiyo hali ya uhuru wa kutenda au kutotenda alionayo mwanaadamu, inatokana na maumbile yake alioumbiwa nayo.

5: Nidhamu ya Kiungu katika mpangilio wa dunia: nidhamu ya kilimwengu imejengeka katika mtindo wa kuathiriana, na kwa kupitia msingi huo (wa kuathiriana) kila kitu huwa kinaathirika kutokana na kitu fulani, pia vile vile kinaweza kukiathiri kitu chengine na kusababisha kutokea tokeo fulani. Na huo ndio mfumo maalumu uliowekwa na Muumba kwa ajili kuuendesha ulimwengu huu. Katika suala la uongofu, Mola Mtakatifu amezitayarisha sababu maalumu zitazomfanya kila mpenda haki kuufikia uongofu wa Mola wake hii ni kwa ajili ya kumrahisishia mja wake kuyafikia malengo ya kuumbwa kwake kwa urahisi.

Kwa baraka za Aya tulizozitaja pamoja nukta mbali mbali zilizopita, tumeweza kufahamu kuwa muongozo wa kimaumbile unakihusu kila kiumbe akiwemo mwanaadamu, tusisahau pia mwanaadamu huyu amepewa nyongeza ya uongofu wa kisheria. Pia zingatia kuwa: ingawaje yeye amepewa muongozo wa kisheria, lakini bado muongozo huo haumkalifishi yeye kutenda matendo yake kinyume na matakwa yake, bali yeye atabaki kuwa huru katika kutenda matendo hayo, na hilo linatokana na uhuru wa kimaumbile aliokuwa nao. Naye vile vile yuko huru katika kuutafuta muongozo wa kisheria na kuufuata, au kulifumbia macho jambo hilo na hatimae kuidhulumu nafsi yake kwa kule kuizuia na kuifanya isiufikike muongozo huo. Mola Mtukufu alikuwa anao uwezo wa kumpa mja wake uongofu wa lazima na kumfanya yeye atende matendo yake bila ya hiyari yake, lakini Mola alitaka mwanaadamu awe huru ndio maana akampa akili ya kulibaugua jema na baya na kumtaka yeye atende mema kwa manufaa yake na jamii yake, jambo ambalo lingelimfanya yeye kuufikia ukweli halisi wa ubinadamu wake.

Natija ya utafiti:

Sasa itakuwa imeshaeleweka kuwa usemi wa kusema kwamba; Mola Mtakatifu hakutaka waja wake waongoke, si usemi sahihi, bali ukweli uko kinyume na usemi huo, kwani Mola Mtukufu amemtaka kila mmoja kuufikia uongofu wake. Ila tu Yeye amemuekea mwanaadamu nidhamu maalumu ya kuufikia uongofu huo, na nidhamu hiyo ni kule kumfanya mwanaadamu auendee uongofu huo kwa uhuru na hiyari yake mwenyewe. Na wala muongozo wa kisheria haumuandami yeye kimaumbile na kumtoa katika hali ya uhuru alionao,[9] elewa pia; iwapo yeye atatembea ndani ya uwanja wa haki, hapo ndipo atapopata taufiki zaidi ya kuifikia hidaya ya Mola wake.[10]

Mola Mtukufu anasema: “والذين جهدوا فينَا لَنَهدِ ينَّهم سُبلَنا وَ إنّ اللَّه لَمع المحسنين

Maana yake ni kwamba: “Na wale wenye kufanya jitihada kwa ajili yetu, kwa yakini Sisi tutawaongoza (na kuwaonyesha) njia zetu, na bila shaka Mola yu pamoja na watenda hisani”.[11] [12]

 


[1] Suratu Sijda Aya ya 13.

[2] Suratu Taaha.

[3] Suratul- A’alaa Aya ya 2 hadi 3.

[4] Aya ya 30 ya Suratul-A’araaf.

[5] Suratul-Baqara Aya ya 213.

[6] Suratul-Kahf Aya ya 29.

[7] Suratul-Insaan Aya ya 3.

[8] Rejea kitabu Mathnawiy Mawlawiy cha Jalaalu-Diin Muhammad Balkhiy.

[9] Rejea Suratul- Baqara Aya ya 264, Maaida Aya ya 67, Tauba Aya ya 37 na ya 80.

[10] Rejea Aya hizo hizo.

[11] Nyenzo zilizotumika katika kulijibu swali hili ni:

Chapa ya tatu ya mwaka 1262 Shamsia  ya Tarjuma ya Tafsiir Al-miizaan ya Muhammad Husein Tabaatabaai iliochapwa na Muhammady, juz: 14, uk: 214 na kuendelea. Juz: 1, uk:66 na kuendelea. Juz: 17, uk: 167 na kuendelea. Juz: 32, uk: 89 na kuendelea. Vile vile Tafsiri Nemune ya Makarim Shirazi  juz: 1, uk: 67 na uk: 430. juz: 2, uk: 259 na kuendelea. Juz: 17, uk: 166 na kuendelea. Juz: 25, uk: 336 na kuendelea. Juz: 11, uk: 365 na 223 hadi 226 uk: 420 na kuendelea.

[12] Suratu Ankabuut Aya ya 69.

 

TARJAMA YA JAWABU KATIKA LUGHA NYENGINE
MAONI
Idadi ya maoni 0
Tafadhali ingiza thamani
mfano : Yourname@YourDomane.ext
Tafadhali ingiza thamani
<< Niburute.
Tafadhali ingiza kiasi sahihi ya usalama Kanuni

MPANGILIO WA KIMAUDHUI

MASWALI KIHOLELA

YALIYOSOMWA ZAIDI