Please Wait
13331
Kuna hali tatu za kimiujiza zilizotajwa kuhusiana na muujiza wa Qur-ani: muujiza unaohusiana na maneno ya Qur-ani, muujiza wa yale yalioomo ndani yake na muujiza wa Yule aliyekuja na Qur-ani (s.a.w.w)
- Muujiza unaohusiana na maneno ya Qur-ani umegawika katika sehemu mbili:
A- Muujiza wa kibalagha:
Qur-ani katika ubainishaji wake wa mambo mbali mbali imetumia mtindo pekee ulio bora zaidi kuliko aina zote zile za ubainishaji wa wanaadamu, kiasi ya kwamba hakukutokea mtu hata mmoja aliyeweza kufanya upinzani na Qur-ani kuhusiana na hilo, na hata maneno ya mtume (s.a.w.w) ambayo hujulikana kwa jina la hadithi takatifu, hayawezi kulingana na Qur-ani katika mtindo wake. Kwa hiyo yale madai ya wale waliojaribu kuwazuia masahaba kuziandika hadithi za mtume (s.a.w.w), eti kwa kukhofia kuchanganyika kwa Qur-ani na hadithi, hayawezi kukubalika katika hali yeyote ile
.
B- Muujiza wa Kihesabati na kiadadi:
Katika ulimwengu wa leo kumetumika juhudi kubwa kwa kutumia fani ya compyuter katika kutafuta fungamano la kiadadi lililopo baina ya maneno na herufi zilizomo ndani ya Qur-ani, utafiti ambao umeweza kuonesha umahiri ambao hauwezi kupatikana katika maneno yeyote yale yatokayo kwa mtu wa kawaida.
- Muujiza wa yale yaliomo ndani ya Qu-rani waweza kugawika katika aina zifuatazo:
- Muujiza wa kuto kuwepo khitilafu miongoni mwa yale yaliomo ndani yake.
- Muujiza katika utowaji wa habari kuhusiana na mambo yajayo, na miongoni mwayo kuna yale ambayo tayari yameshaonekana kutokea.
- Muujiza wa kielimu ambao unazihusu elimu mbali mbali zinazoweza kuonekana ndani yake, elimu ambazo zilikuwa ni ngeni katika zama zile za zamani, na elimu hizo zilikuja kuwafumbua macho wanaadamu katika nyanja mbali mbali za kiutambuzi, Kifalsafa, kiakili n.k.
- Muujiza wa kuto patikana fani yeyote ile hadi kufikia zama za leo iliyoweza kuipiku mitazamo na misingi mbali mbali ya kielimu iliyothibitishwa na Qur-ani tukufu.
- Muujiza kwa upande wa Yule aliyekuja na Qur-ani hiyo (s.a.w.w):
Mtume (s.a.w.w) ambaye alikuja na Qur-ani, alikuwa ni mtu aliyekuwa hakusoma elimu ya kusoma na kuandika, wala elimu nyengine yeyote ile kutoka kwa watu au mtu fulani, iweje basi mtu wa aina kama hiyo aweza kuja na kitabu kama hichi bila kuwepo miujiza ya Mola Mtakatifu?
Kumetolewa ufafanuzi wa aina mbali mbali kuhusiana na aina za miujiza ya Qur-ani[1], miujiza ambayo tunaweza kuigawa katika sehemu tatu kuu zifuatazo:
- Muujiza unaohusiana na maneno ya Qur-ani
- Muujiza unaohusianan na yale yaliyomo ndani ya Qur-ani
- Muujiza unaohusiana na Yule aliyeteremshiwa Qur-ani hiyo
Muujiza unaohusiana na maneno ya Qur-ani:
Muujiza unaohusiana na maneno ya Qur-ani umegawika ndani ya vipengeke viwili, navyo ni: muujiza wa kibalagha na muujiza wa kiadadi unaohusiana na elimu ya Hesabati.
Muujiza wa kibalagha uliomo ndani ya maeno ya Qur-ani ni muujiza maarufu uliotambulikana tokea zama za zamani, na hakuna upinzani unao onekana kuhusiana na muujiza huo katika mitazamo mbali mbali ya wanazuoni wa madhehebu mbali mbali. Bali tu kuna wanazuoni wengine ambao wanaoona kuwa: “muujiza wa kibalagha ni wenye kupambanuka na ule muujiza wa kimpangilio na muujiza wa namna ya uzuri wa kimaelezo unaopatikana ndani ya Qur-ani”,[2] huku wanazuoni wengine wakiyahesabu yote hayo kuwa ni aina moja tu ya muujiza uliyopambika kwa rangi tofauti, ujulikanao kwa jina la muujiza wa kibalagha, kuuhesabu muujiza wa kibalagha kuwa uko nje ya muujiza wa kimpangilio na kimaelezo, huwa ni moja kati ya kutoa ufafanuzi tu kuhusiana na muujiza wa kibalagha, kwani mambo yote hayo mawili ni yenye kufungamana na muujiza wa kibalagha na wala hayako nje ya muujiza huo, kiasi ya kwamba kila mmoja uwe ni wenye kuhesabiwa kuwa ni muujiza wa aina yake. Muujiza wa kibalagha ni muujiza ambao hauwezekani kuonekana ndani ya maneno ya mtu yeyote yule, hata ndani ya hadithi za Mtume (s.a.w.w).
Tukiizingatia tarehe inayohusiana na elimu ya hadithi, tutawakutia wanazuoni waliodai kuwa: “Mtume (s.a.w.w) alilipigia marufuku suala la uandishi wa hadithi”, huku wakizinukuu baadhi ya hadithi zitokazo Kwake (s.a.w.w) kuhusiana na jambo hilo,[3] lakini wao katika usemi wao huo ni lazima wakabiliwe na swali lisemalo kuwa: “ni jambo gani lililomfanya Mtume (s.a.w.w) kupiga marufuku uandishi wa hadithi?”
Moja kati ya jawabu zilizotolewa ambayo ni jawabu maarufu katika madhehebu ya kisunni, ilisema kuwa: “upigaji marufu kuhusiana na uandishi wa hadithi ulikuja kwa ajili ya kuepusha tatizo la kuchanganyika maandiko ya Qur-ani na yale yasiyokuwa Qur-ani, yaani hadithi za Mtume (s.a.w.w). Mmoja kati ya wanazuoni wa kisunni asiyekubaliana na uoni huo alijibu kwa kusema: “balagha iliyomo ndani ya Qur-ani ni ngao tosha ambayo ni kinga inayoweza kuyapambanua kwa urahisi kabisa maandiko ya Qur-ani na yale yasiyokuwa Qur-ani (hadithi)”[4], alisema hayo kisha akaendelea kuutatua utata unaotarajiwa kusema kuwa: “pengine Mtume (s.a.w.w) Naye anaweza kuzungumza maneno yatakayokwenda sambamba kibalagha na maneno ya Qur-ani” mwanazuoni huyu akiujibu utata huu alisema: “iwapo tutakubaliana na usemi huo, hapo basi tutakuwa tunapingana na ule usemi wetu usemao kuwa: (Qur-ani ni yenye muujiza wa kibalagha ushindao maneno mengine yote yale yasiyokuwa Qur-ani)”.[5]
Hivyo basi suala la kuwazuia watu wasiziandike hadithi kwa madai ya kukhofia kutokea mchanganyiko baina ya Qur-ani na hadithi za Mtume (s.a.w.w), ni moja kati ya maswali yanayotakiwa kupatiwa ufumbuzi kutoka kwa ndugu zetu wa kisunni, na ingawaje sisi hatuyahesabu maneno ya Mtume (s.a.w.w) kuwa ni sawa na maneno ya watu wa kawaida, bali ni maneno yenye nuru ambayo chanzo chake ni Wahyi utokao kwa Mola wake (s.w), huku sisi tukiwa ni wenye kuwategemea maneno hayo katika kuyapatia ufumbuzi masuala mbali mbali ya kisheria na kijamii, lakini bado tunaamini kuwa: kuna tofauti kubwa ya kibalagha iliyopo baina ya maneno ya Mtume (s.a.w.w) na yale ya Mwenye Ezi Mungu (s.w), na wala hakuna hata mwanazuoni mmoja miongoni mwa wanazuoni wa kishia mwenye mtazamo usemao kuwa: Mtume (s.a.w.w) alilipigia marufuku suala la uandishi wa hadithi.
Aina nyengine ya muujiza wa Qur-ani, ni muujiza wa kiadadi, yaani mpangilio na fungamano la Kihesabati lililomo ndani yake, watafiti mbali mbali walilifanyia kazi suala la kuwepo kwa fungamano hilo mnamo miaka ya karibuni kwa kupitia fani ya compyuter, na hatimae kukagunduliwa kuwa kuna fungamano madhubuti la Kihesabati lililopo baina ya maneno ya Qur-ani na herufi zilizomo ndani yake, fungamano ambalo huwa halipatikani ndani ya maneno ya watu wa kawaida.[6]
Muujiza unaohusiana na yale yaliomo ndani ya Qur-ani
Muujiza uhusianao na yale yaliomo ndani ya Qur-ani, umeelezewa kwa kupitia mitindo mbali mbali, miongoni mwayo ikiwa ni kama ifuatayo:
A- Kutopatikana mgongano kuhusiana na yale yaliomo ndani yake:
Ndani ya Qur-ani mna Aya zilizo wazi kabisa katika kulithibitisha hilo, na moja kati ya Aya hizo ni ile isemayo:
“ أ فلا يتدبرون القرآن و لو كان من عند غير الله لوجدوا فيه اختلافاً كثيرا”
Maana yake ni kwamba: “Hivi hawaitafakari hii Qur-ani, kwani ingalikuwa inatokana na asiyekuwa Mola (wa haki) basi wangalikuta ndani yake aina mbali mbali za migongano pamoja na kuto kuwepo muowano ndani ya Aya zake”[7].
B- Muujiza katika utoaji wa habari na bishara za mambo yatakayotokea baadae:
Qur-ani imetoa habari mbali mbali za matokeo ya baadae, matokeo ambayo ima yalikuwa yanahuisiana na mtu, tabaka fulani au pia mambo mbali mbali ya kielimu n.k. Na mambo hayo yaliweza kuonekana bayana kabisa kama vile yalivyobashiriwa na Qur-ani.
Baadhi ya matokeo yaliyobashiriwa na Qur-ani kutokea, ni lile tokeo la kushindwa kivita dola la Kirumi, huku kukitolewa bishara ya kushinda kivita dola hilo baaya kipindi cha muda usio mrefu. Mola Mtakatifu kuhusiana na hilo Anasema:
“ا لم* غلبت الروم فى أدنى الارض و هم من بعد غلبهم سيغلبون ”
Maana yake ni kwamba: “Alif Lam Miym. Warumi wameshindwa. Wameshindwa katika mapigano yaliyotokea kwenye nchi iliyo bondeni zaidi (chini kabisha) mwa sayari ya dunia (nako ni Jerusalem), nao basi baada ya kushindwa kwao watashinda (katka kipindi cha baadae)”[8]
C- Muujiza wa Qur-ani kuhusiana na elimu mbali mbali:
Kuna masuala mbali mbali ya kielimu yaliyozungumziwa ndani ya Qur-ani, na ilikuwa ni jambo la muhali na lisilowezakana ndani ya zama za Mtume (s.a.w.w), kuweza kupatikana mtu aliyekuwa na ujuzi wa kuyatambua masuala hayo. Na bado kuna mengi ambayo hadi leo hawajatokea wajuzi wa kuyatambua na kuyafafanua ipaswavyo, isipokuwa mfafanuzi wa hayo ni Mtume tu (s.a.w.w) pamoja na maimau waongofu (a.s). Kwani kuna hadithi tofauti zilizogusia na kuzungumzia masuala tofauti ya kiakida, kiakili pamoja na Kifalsafa, yaliyobeba ujumbe mzito ndani yake jambo ambalo huwa linahitajia msada kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) pamoja na maimamu ili kufahamika ipaswavyo masuala hayo. Na hata kama kutadaiwa kuwepo kwa watu mbali mbali waliyo weza kuyapatia ufumbuzi masula mbali mbali ya kielimu yaliyomo ndani ya Qur-ani na hadithi, lakini hilo halikuwa ni jambo lililoweza kupatikana kabla ya zama hizi, bali hilo limethibitika kwa kule kuwepo aina mbali mbali za ufafanuzi wa Mtume (s.a.w.w) pamoja na maimamu (a.s) kwa njia moja au nyengize, ufafanuzi ambao ulikuwa ni chanzo na msukumo tosha kwa watafiti mbali mbali kuweza kuyafikia yale waliyoweza kuyafikia. Na kuwepo kwa watafiti walioweza kuyatambua baadhi ya yale yaliomo ndani ya Qur-ani, huwa si jambo lenye kuipunguza tahamani ya muujiza huo wa kielimu uliomo ndani ya Qur-ani. Pia ni muhimu kuzingatia kuwa: muujiza huu wa kuyazungumzia mambo mbali mbali ya kielimu, hautokani na Mtume (s.a.w.w), bali ni fani maalumu iliyotoka kwa Mola mtakatifu na kumshukia Mjumbe Wake (s.a.w.w).
D- Muujiza wa kushindwa watu tofauti kuyapiku yale yaliyomo ndani ya Qur-ani:
Miaka mingi imepita huku wanaadamu wakipiga hatua katika fani tofauti za kielimu, lakini hadi leo hakukutokea mtu aliyeweza kuyapiku yale yaliyomo ndani ya Qur-ani, jambo ambalo huwa ni msingi mkuu katika kuuthibitisha ukweli na umadhubuti wa Qur-ani pamoja na umahiri wa Mola Mtukufu. Ni muhimu kuzingatia kuwa: vile vile kuna elimu kama vile Hesabati na Mantiki, ambazo ni elimu za kale zilizothibiti bila ya kupatikana mageuzi ndani yake, hii ni kwa kutokana na kuwa elimu hizo ni elimu ziendazo sambamba na akili madhubuti ya mwanaadamu, na kila mmoja wetu ni mwenye kuidiriki mifumo ya elimu hizo kifitra, kimoyo na kimaumbile. Lakini pia inatakiwa kufahamika kwamba, waliokuja kuziandika na kuzipanga elimu hizo, hawakuwa ni wavumbuzi, bali walikuwa ni wakusanyaji tu wa elimu hizo zilizomo ndani ya akili ya kila mmoja wetu, ingawaje kuzitambua elimu hizo huwa kunahitajia aina fulani ya mzinduko wa kiakili, kutokuwa na mzinduko huo haukumaanishi kuwa: yule asiyekuwa na mzinduko huo huwa si mwenye kuzimiliki elimu hizo ndani ya akili yake. Vile vile zingatio la pili kuhusiana na hilo ni kuwa: kitabu kinachoandikwa na mwanaadamu huwa kinagusia elimu moja maalumu iliyozingatiwa ndani ya kitabu hicho, hali ya kuwa Qur-ani takatifu imezungumzia elimu mbali mbali bila ya kupatikana dosari ndani yake wala pingamizi. Juu ya yote hayo tuliyoyazungumzia, pia bado Qur-ani itakuwa ni bingwa pekee katika kuzitambulisha elimu tofauti na kuyaelezea masuala mbali mbali ya kielimu, huku kukiwa na fungamano kamili liendalo sawa sawa na maelezo hayo pasi na kupatikana dosari ya aina yeyote ile ya kilugha, kifasihi na kimaana, au pia kupatikana mgongano ndani bayana zake. Ni nani basi miongoni mwa wanaadamu awezaye kutoa aina kama hiyo ya ufafanuzi wa mambo bila ya kujikanyaga au kupata upinzani utakao yapiku maelezo yake? Chunguza, zingatia na fahamu kwa makini ukweli huo.[9]
3- Muujiza utokanao na Yule aliyekuja na Qur-ani:
Muujiza huu ni muujiza uliozingatiwa na watu tofauti tokea zamani, mazingatio ambayo yaligusia suala zima la Mtume (s.a.w.w) ambaye alikuja na Qur-ani huku akiwa Yeye si mwenye kujua kusoma wala kuandika, basi vipi mtu kama huyu aliyekuwa na sifa kama hizo ambaye aliishi ndani ya jamii isiyobobea kielimu wala kitamaduni, aweze kuja na kitabu kama hichi bila ya kupata msada utokao kwa Mola wake?[10]
Suala la utafiti kuhusiana na miujiza ya Qur-ani linahusiana zaidi na elimu ya Akida, inagawaje katika elimu ya Fani za Qur-ani pia suala hili limefanyiwa aina mbali mbali za utafiti ndani yake.[11]
Kwa ufafanuzi zaidi waweza kusoma kitabu cha mabani kalaamiy ijtihadi cha Mahdi Haadawiy Tehraaniy, chapa ya kwanza iliyochapishwa na Muasese farhangiy khaaneye khirad Qum, mwaka 1377 Shamsia.
[1] Angali a makala yanayohisiana na aina ya miujiza ya Qur-ani ya Sayyid Mustafa yaliyotayarishwa kwenye semina ya pili inayohusiana na utafiti juu ya Qur-ani na fani zake chapa ya Darul-Qur-ani Qum Iran, uk: 178-168.
[2] Rejea makala yaliyopita, uk: 169.
[3] Rejea kitabu adhwa-a alaa sunnatil-Muhammadiyya cha Abu Rayya, uk: 42.
[4] Kitabu kilichopita, uk: 46.
[5] Kitabu hichi hicho, uk: 47.
[6] Kuhusiana na hilo kuna software maalumu iliyotayarishwa na dokta Sayyid Ali Qaadiri iitwayo (qadar).
[7] Suratun- Nisaa, Aya ya 82.
[8] Suratu Ruum, Aya ya 1-3.
[9] Imenukuliwa kutoka kwa Allaama Tabaatabaai kwamba: “yale yote yaliyomo ndani ya Qur-ani yanaweza kutolewa katika kila Sura moja ya Qur-ani” na kama hali itakuwa ni kama hiyo basi itamaanisha kuwa, mfumo wa Aya tofauti unaojenga Sura moja ya Qur-ani, utakuwa ni wenye kuyaelezea yale yote yaliyokuja ndani ya Qur-ani nzima, na hiilo litamaanisha kuwa, mafunzo yote ya kielimu yalyiomo ndani ya Qur-ani, yatakuwa yamekaririwa mara 114 kwa kupitia aina mbali mbali za kiufafanuzi ndani ya Sura 114.
[10] Baadhi ya wanazuoni wa Kimagharibi wamijibu hoja hii kwa kusema kuwa: Mtume (s.a.w.w) alikuwa na elimu, elimu ambayo aliipata kutoka kwa wanazuoni wa dini zilizopita, na kwa kupitia elimu hizo aliweza kuandika kitabu cha Qur-ani, na kule watu wa Makka kusifiwa ndani ya Qur-ani kuwa walikuwa ni wajinga haimaanishi kuwa wao hawakuwa na elimu, bali wao hawakuwa na elimu kuhusiana na Mungu, kwani Makka kulikuwa watu wengine waliokuwa na elimu za hali ya juu, na kwa upande mwengine Yeye mwenyewe (s.a.w.w) alijulikana kuwa ni mtume miongoni mwa wasiojua kusoma na kuandika, kwa sababu ya Yeye (s.a.w.w) kuwa ametokana na jamii ya aina hiyo, waliokosa elimu ya Mola wao. Lakini yote hayo ni maneno yasiyo na msingi madhubuti, ila tu malengo yalikuwa ni kuukanusha muujiza wa Qur-ani, rejea kitabu uluumul-hadith wa mustalahaatuhu, uk: 2-3 cha dokta Subhi Saaleh.
[11] Rejea kitabu mbani kalaamiy ijtihaadi cha Mahdi Hadawiy Tehraaniy, uk: 47-51.