Please Wait
12657
Kuna baadhi ya Riwaya na Hadithi zilizopokelewa kutoka kwa baadhi ya Maimamu (a.s) zenye kuashiria suala hilo.
Lakini hakuna ajabu kuhusiana na suala hilo, kwani Mwenye Ezi Mungu aliwanusuru mitume tofauti pamoja na mawalii wake kwa kuwapelekea msaada wa majini na Malaika, kwa hiyo hilo si suala geni lenye kuweza kuwashangaza watu, Mola Mtukufu anamwambia Mtume wetu (s.a.w.w): “kumbuka ule wakati ambao mlikuwa katika matatizo makubwa pale mlipokuwa katika vita vya Badri, huku mkimuomba Mola msaada, Naye akakukubalieni maombi yenu, akakuambieni, mimi ninakusaidieni kwa kukushushieni jeshi la Malaika elfu moja.” Ama sababu zilizomfanya Imamu Husein (a.s) kuukataa msaada huo ni kama zifuatazo:
- Kuuliwa kwake yeye katika uwanja ule wa Karbala ilikuwa ndio njia pekee itakayaweza kuuhuisha Uislamu kwa mara nyengine.
- Shauku kubwa ya Imamu Husein (a.s) ya kutaka kuonana na Mola wake.
- Kuuwawa kwake Yeye (a.s), kulikuwa ni jambo la lazima.
- Yeye (a.s) kufa shahidi kulikuwa ndio jambo pekee la ufakhari litakalompa Yeye (a.s) cheo mbele ya Mola wake.
Msaada kotoka kwa Mola kwa ajili ya Imamu Husein (a.s)
Kuna baadhi ya Hadithi na Riwaya kutoka kwa Maimamu (a.s) zinazoashiria kuwa, Imamu Husein (a.s) ajiwa na Malaika pamoja na majini wakitaka kumpa msaada, lakini Yeye (a.s) aliukataa msaada huo, miongoni mwa Riwaya hizo ni ile Riwaya iliyopokelewa kutoka kwa Imamu Saadiq (a.s) iliyosema kuwa: pale Imamu Husein (a.s) alipofunga safari kutoka Madina akielekea Karbala, alijiwa na kundi la Malaika waliokuja kumpa ushauri wa kumpa msaada, na pia kulikuwa na gurupu kubwa la majini waliokuwa Waislamu ambao walikuja kutaka kumsaidia, lakini Yeye (a.s) aliwajibu kwa kuwaambia: “Mungu akulipeni jaza njema, kwa kweli mimi ndiye mhusika na mkusudiwa wa vita hivi, na tayari wakati na sehemu nitakayouliwa imeshatambulikana.” Majini wakasema: “Ingelikuwa si hiyari yako mwenyewe basi tusingembakisha adui hata mmoja katika vita hivi.” Naye (a.s) akawajibu kwa kusema: “sisi wenyewe tungalikuwa na nia ya kufanya hivyo, basi tungelifanya kwani sisi ni wenye uwezo zaidi juu ya hilo, lakini sisi hatuna haja ya kufanya hivyo, kwani kila mmoja anayetaka kupotoka basi apotoke kwa hiari yake huku tukiwa sisi tumeshawafunulia dalili za wazi zitakazowanyima wao hoja za kujitetea siku ya Kiama mbele ya Mola wao, na wenye kuitaka haki nao waifuate kwa uoni ulio wa wazi ya kufichika kitu au kupata ukanganyifu”.[1] Vile vile Imamu Saadiq (a.s) amesema: ‘nimemsikia baba yangu akisema: pale Imamu Husein (a.s) alipokutana na Omar bin Sa’ad katika kuanza baina yao, Mola aliituma nusra yake, nusra ambayo ilikuwa ni hiyari kwa kuitumia ili awashinde adui zake, au kuto itumia na kukubali kukutana na Mola wake, hivyo basi Yeye (a.s) alikubali kuto itumia kwa ajili ya kuonana na Mola wake”.[2]
Na si Riwaya hiyo tu iliyoelezea suala hilo, bali kuna Riwaya nyengine mbali mbali, kama ile isemayo kuwa: Malaika walimjia Imamu Husein (a.s) na kutaka kumpa msaada wa kivita, Naye (a.s) mwanzo aliwakatalia, nao wakarudi, na kwa mara yapili walivyokuja kutaka kumpa msaada wakamkuta tayri ameshauwawa. Riwaya iliyopokelewa kutoka kwa Imamu Saadiq (a.s) inasema kuwa: “walikuja Malaika elfu nne ambao walishuka kwa ajili ya kumpa Yeye (a.s) msaada, lakini Yeye (a.s) akawakatalia, kisha wakenda kwa Mola wao kutaka idhini ya kuja kwa mara ya pili, lakini alipokuja walimkuta tayari ameshauwawa… .”[3] Kwa ufupi ni kwamba kuna Riwaya zenye kuashiria suala hilo, na ni Riwaya zilizokubalika mbele ya wanazuoni, na wala hakuna mwanachuoni aliyezikanusha Riwaya hizo au kuzikataa, kwani hakuna uchafuzi au upotoshaji unaoweza kutokea katika dini iwapo mtu atazikubali Riwaya hizo. Na si hilo si jambo la ajabu, kwani si mara moja wala mbili Mwenye Ezi Mungu aliwatumia wajumbe na mawalii wake aina mbali mbali za misaada itokayo kwake, iwapo utaiangalia Qur-ani kwa makini utazikutia Aya mbali mbali zinazoelezea ukweli huo, na miongoni mwa Aya hizo ni ile isemayo: “Kumbukeni pale mlipomtaka msaada Mola wenu (katika vita vya Badri) na Mola wenu akakukubalieni maombi yenu (akakuambieni) Mimi ninakusaidieni kwa kushushieni jeshi la Malaika elfu moja mfululizo.[4] Vile vile kuna misaada mbali mbali walioipata Waislamu kutoka kwa Mola wao pale walipokuwa wakipambana na adui zao, kama vile msaada waliopewa walipokuwa katika vita vya Ahzaab na mengineyo, misaada hii ilikuwa ikitolewa kupitia majini na Malaika, na misaada hii inaweza kutopatikana kwa sababu ya maslahi maalumu ambayo tutaitaja hivi karibuni.
Hivi ni kwa nini Imamu Husein (a.s) alikataa kupokea msaada wa majini na Mlaika?
Swali hili laweza kujibiwa kama ifuatavyo: yawezekana Yeye (a.s) aliikataa misaada hiyo kwa sababu zifuatazo:
- Kwa kuzingatia hali nzima ya kisiasa iliokuwepo katika zama zile, siasa ambayo ilitengenezwa na Muawia pamoja na mwanawe Yazidi kwa ajili ya kuipotosha dini, ikuwa ni vigumu mtu kutofautisha haki na batili, kwa jinsi ya mkorogeko ulioletwa na watu hawa wawili ulivyoichafua dini ya Mola, hivyo basi kulikuwa hakuna budi Imamu Husein (a.s) na masahaba kujitoa muhanga kwa ajili ya kuifufua dini hiyo kwa mara nyengine tena.[5]
- Kilichothibitika katika Riwaya mbali mbali ni kuwa, kuuwawa kwa Imamu Husein (a.s) lilikuwani jambo lisiloepukika, kwani hiyo ilikuwa ndiyo nia yake halisi pale alipoelekea vitani, huku akiwa na hamu ya jambo hilo kwa ajili ya kuihuisha dini ya Mola Mtukufu, ili kufanya kwake hivyo kuwe ni fakhari mbele ya Mola Wake, jambo ambalo litakuwa ni lenye kumpandisha yeye katika daraja za juu kabisa.[6]
- Imamu Husein (a.s) alikuwa akiyathamini sana mauti kwa ajili ya Mola wake, na hakuyaona mauti bora kuliko hayo, Yeye mwenyewe (a.s) alilizungumzia na kulisifia pale alipokuwa akiondoka Makka kuelekea Iraq kwa kusema: “Medali ya mauti kwa mwanaadamu ni kitu chenye kuvutia mno kama vile kidani cha harusi kinavyomvutia biharusi”.[7] Usemi huu unatufahamisha kuwa, mauti si mtego wala mashaka yanayomlazimu mtu bali ni medali na pambo kwa wacha Mungu, ni kwa nini basi mtu asiamue kuivaa medali hii kwa ajili ya kukutana na Mola wake?!, mauti mbele ya Imamu Husein (a.s) hayakuwa ni shubiri, bali yalikuwa ni asali hasa pale mauti hayo yalipomjia katika njia ya shahada kwa ajili ya Mola wake.[8]
Mtu kufa shahidi si upungufu, kiasi ya kwamba mtu atafute njia ya kulikimbia jambo hilo, au atafute msaada kutoka kwa Malaika utakaomzuia yeye asikutane na jambo hilo, bali kufa shahidi ni sifa muhimu yanye kumpandisha mtu daraja, nabii Ibrahim (a.s) alilielewa hilo tokea mwanzo, ndiyo maana pale alipotupwa kwenye shimo la moto aliukataa msaada wa Jibrail (a.s) na wala hakumtaka yeye amsaidie kwa hali yeyote ile, kwa mawalii wa Mola siku zote na wakati wote huwa wanatamani kukutana na Mola wao huku wakimtakasa nyakati zote.[9]
- Kukutana na Mola pamoja na mitume na mawalii mbali mbali walioko mbele ya haki, lilikuwa ni jambo muhimu alilokuwa akilitamani sana Imamu Husein (a.s) kwa Yeye (a.s) alikuwa akiwapenda watu wena na mawalii wa Mungu, kwani iwapo utaisoma hutuba yake aliyoitoa alipokuwa Makka akielekea Karbala, uta,kutia Imamu (a.s) akisema: “Mapenzi ya kutaka kukutana na watu wema wa kizazi changu ambao wako mbele ya haki, ni yenye mvuto mkubwa kama vile mvuto wa mapenzi ulioko baina ya nabii Yusuf na nabii Yaaqoob”.[10]
- Imamu Husein (a.s) hakutaka kutumia njia za kiiujiza kwa ajili ya kupambana na adui zake, kwa Yeye (a.s) alikuwa na uwezo wa kutumia njia za kimiujiza kwa ajili ya kuwtokomeza adui zake bila hata ya kuomba msaada kutoka kwa Malaika au majini, lakini kufanya hivyo kulikuwa ni njia ilio nje ya ulimwengu wa dhahiri unaodirikiwa na kila mmoja, Naye (a.s) alitaka kukabiliana nao kwa kupitia nguvu zake za kimwili bila ya kutumia nguvu za kiroho. Imamu Husein (a.s) aliheshimika kutoka katika pande zote mbili, za Waislamu na wasiokuwa Waislamu, na kilichomfanya aheshimike, ni kule kuwa yeye ni mpiganiaji wa uhuru aliyekuwa akitumia nguvu zake za kawaida katika suala hilo na katika masuala mengine ya kisiasa na kijamii na sio nguvu za kiroho. Yeye (a.s) aliamua kukipeleka kizazi chake chote vitani ili jambo hilo liwe ni zinduo litakalozizindua aikili za Waislamu na kuwafanya wao waitetee dini yao pamoja na uhuru wao binafsi, na hilo ndilo lililothibiti baada ya matokeo ya vita vya Karbala, kwani mapinduzi ya Imamu Husein yameweza kubakia milele hadi leo. Je Imamu Husein (a.s) hakuwa na uwezo wakutumia nguvu za ghaibu kwa ajili ya kuwashinda adui zake? Akili kichwani mwako, kwani tayari sisi tumeshatoa ufafanuzi wa kutosha kuhusiana na suala hilo.
[1] Biharul-Anwaar cha Allaama Majlisiy, juz/44, uk330, chapa ya Muasastul-Wafaa, Beirut, Lebanon.
[2] Luhuuf cha Sayyid bin Taawuus, uk/141, kilichofasiriwa kwa Kifarsi na Abu Taalibiy Sayyid Abul-Husein, chapa ya kwanza ya Dalile maa, Qum Iran, mwaka 1380 Shamsia.
[3] Rejea tarjama ya kitabu Aamaaliy cha sheikh Saduuq kilicotarjumiwa na Muhammad Baaqir Kamreiy, uk/638, chapa ya sita ya Islaamiyya Tehran ya mwaka 1376 Shamsia, pia kuna Riwaya katika kitabu (Alkaafiy) cha marhum Koleiniy yenye kufanana na Riwaya hii, rejea (Alkaafiy), juz/1, uk/283 hadi 284.
[4] Suratul-Anfaal, Aya ya 9.
[5] Rejea kitabu (Aazakheshiy diigar az aasimaan Karbala) cha Muhammad Taqiy Misbah Yazdiy, uk/ 44 hadi 66, chapa ya tano ya Muasese amuzeshiy wa pazuheshii imam Khomeini, mwaka 1380 Shamsia.
[6] Rejea kitabu (Biharul-anwaar), juz/44, uk/329.
[7] Rejea kitabu (Biharul-anwaar), juz/44, uk/366, pia (Kaashiful-ghumma fii maarifatil-Aimma) cha Muhaddith Ardebiiliy, juz/2, uk/29, chapa ya kwanza ya Bani Haashimiy, Tabriz Iran ya mwaka 1381 Shamsia, pi rejea (luhuuf), uk/110 hadi 111.
[8] Rejea kitabu (Shekufae aqli dar partoe nehdhate Huseiniy), cha AbduLlahi Jawadi Aamuliy, uk/28 hadi 30, chapa ya tano ya Israa ya mwaka 1387, Qum Iran.
[9] Rejea kitabu (Shekufae aqli dar partoe nehdhate Huseiniy), uk/27.
[10] Rejea kitabu (Biharul-anwaar, juz/44, uk/366, pia (Kaashiful-ghumma fii maarifatil-Aimma), juz/2, uk/29, pia (Luhuuf), uk/110 hadi 111.