Please Wait
8948
Imamu Khomeiniy (r.a), alitilia mkazo sana katika mazungumzo yake ya mara kwa mara ya kwamba: muhanga wa Imamu Husein (a.s), pamoja kuadhimisha siku ya muhanga huo kwa kuandaa vikao vya maombolezo kwa ajili ya kuikumbuka kwa ajili ya kupata somo juu ya tendo hilo la Imamu Husein (a.s), ni jambo linalopaswa kupewa umuhimu na kuhifadhiwa, kwani jambo hilo ni moja kati ya mambo yenye kupiga vita miporomoko mbali mbali ndani ya dini na jamii. Moja kati ibara za Imamu Khomeiniy (r.a) kuhusiana na hilo ni ibara isemayo: “Mkusanyiko wa kuadhiisha tokeo la Ashura kwa njia ya maombolezo maalumu juu ya mashahidi wa Karbala, ni jambo lenye kuleta Baraka nyingi’.[1] Pia alilisisitiza suala hilo kwa kusema: “Mwezi wa Muharram na Safar, ni miezi yenye baraka, miezi ambayo Uislamu umehuika ndani yake, ni wajibu kwetu sisi kuihuisha miezi hii kwa kuomboleza kutokana na misiba ya watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w), kwani maombolezo hayo ndiyo yalioweza kuyadumisha madhehebu ya Ahlul-Bait (a.s) hadi leo. Miezi ya Muharram na Safar ndiyo iliyoupa uhai Uislamu huu. Muhanga wa Sayyidu Shuhadaa (bwana wa mashaidi) (a.s), ni suala moja kuu lililotuokolea dini yetu hadi leo… .[2]
Imamu komeiniy alikuwa akilizungumzia suala hilo ndani ya hutuba zake tofauti, huku akitoa dalili juu ya usemi wake huo, hebu basi tuiangalie hutuba yake isemayo hivi: “ Ndani ya siku za Ashura, au ndani ya mwezi wa Muharram na Safar na pia ndani ya mwezi wa Ramadhani, maadui huwa na khofu ya kuulembea Uislamu maneno ya fedheha na ufedhuli, au kutaka kuivuruga jamii ndani ya masiku kama hayo. Hii inatokana na wao kutambua kuwa ndani ya siku hizo na miezi hiyo, Waislamu huwa wapo chini ya bendera moja ya ibada na maombolezo, huku wanachuoni mbali mbali wakiihudumia jamii kwa kuipa nasaha muhimu, hivyo basi wao wanatambua kuwa: iwapo watataka kuichafua jamii, wanachuoni hao hawatokaa kimya, bali watawazindua wanajamii hao kuhusiana na njama hizo, na hatimae njama zao zitafedhehewa. Wao wanatambua kuwa mikusanyiko ya watu wanao omboleza kifo cha Imamu Husein (a.s), ni mikusanyiko yenye mfumo maalumu wa mshikamano wa sauti moja, watu hao wanapo omboleza mauwaji ya Karbala, damu zao huwa zinawachemka kwa hasira juu ya tokeo hilo, nao huwa na shauku kubwa ya kutaka kuitetea dini yao kama vile Imamu Husein (a.s) pamoja na wafuasi wake walivyofanya. Hivyo basi iwapo kutatokea machafuzi na dhulma ndani ya dini na jamii yao ndani ya wakati huo, wao watakuwa tayari kujitoa muhanga na kuitetea dini na jamii yao. Ndani ya miezi hiyo huwa hakuna haja ya kuwakusanya watu na kuwapigia bomba, bali makundi mbali mbali ya watu ndani ya mikoa mbali mbali, huwa yako tayari kwa ajili ya kupokea ujumbe maalumu kutoka kwa wanazuoni wao. Mmoja kati ya Maimamu (a.s), nafikiria kuwa alikuwa ni Imamu Baaqir (a.s), alikuwa akisema: “Nileteeni mtu wa kunisomea taazia (maombolezo) kwa ajili ya Karbala, ili asome na alie mbele yangu… . Imamu Baaqir hakuwa akifanya hivyo kwa ajili ya malengo ya nafsi yake, bali Yeye (a.s) alikuwa na malengo maalumu ya Kisiasa yaliolenga kuifufua na kuijenga jamii. Wengi miongoni watu waliojisinga (waliojipaka) rangi ya Umagharibi, wanatucheka na kuiita jamii yetu kuwa ni (jamii ya waliaji ovyo), lakini si wao tu bali hata wale watu walio karibu yetu, hawakijui ni kiasi gani cha thawabu anachokipata yule anayewalilia kwa huzuni mashahidi wa Karbala. Wao hawajui kiwango cha thamani ya maombolezo haya, wala hawatambui thamani ya dua zinazo ombwa kwenye vikao hivyo. Vikao hivi ni mfumo maalumu wa kuwakusanya Waislamu na kuwaweka kwenye lengo moja, jambo ambalo huwafanya wao kuwa ni kundi moja kubwa la wanajeshi wa kuitetea dini na haki za wanajamii mbali mbali. Mkusanyiko wa aina kama hiyo huwa una malengo makubwa ya Kisiasa yenye kuwafanya watu kukielekea kitu kimoja muhimu juu yao chenye makusudio ya utetezi wa dini na jamii. Watu wanapokusanyika na kuomboleza, huwa wanapata muamko maalumu wa Kisiasa wenye kuwafumbua macho, na hilo ndilo lengo la Maimamu (a.s) katika kudumisha vikao hivi vya maombolezo, na wala hakutoweza kupatikana jambo litakalowaamsha Waislamu kuliko jambo hili. Wairani walipoamua kuiangusha serikali ya kidhalimu, walivitumia vikao hivyo kuwa ndio nyenzo muhimu ya kuwahamasisha wana jamii na kuwataka wasimame kidete juu ya utetezi haki zao, na wangelikuwa wao hawakupikika vizuri ndani ya chungu cha maombolezo hayo, basi ingelikuwa ni vigumu sana kuweza kufaulu katika mapinduzi yao, kwani wao walihujumiwa kutoka kila pembe, lakini kumbukumbu ya tokeo la Karbala ikawa ndio ngao ya fikra zao kusonga mbele na hatimae kuzifikia nyanja za juu za maendeleo ya Kisiasa na Kiufundi. Vijana wa Kiirani walipofahamu kuwa Imamu Husein (a.s), alijitolea muhanga yeye pamoja na familia yake kwa ajili ya dini na kwa ajili ya kupata ridha ya Mola wao, vijana hao walisonga mbele bila ya woga katika vita vya Sadamu Husein dhidi ya Iran, vijana hao walikuwa na shauku kubwa ya kufa shahidi kama alivyouwawa Imamu Husein (a.s) pamoja na wafuasi wake, jambo ambalo liliwafanya wao wasonge mbele bila ya khofu, na pale mmoja wao alipokuwa hakufanikiwa kufa shahidi, alikuwa akilia na kuhuzunika kutokana na hilo, wazee pia nao walikuwa wakiona fakhari pale waliposikia kuwa mmoja kati ya watoto wao amekufa shahidi, wazazi hao waliposikia kifo cha mtoto wao, bado walikuwa hawarudi nyuma, bali walikuwa wakisema: bado tuna mtoto mwengine, na kama kutahitajika wanajeshi, basi sisi hatuna upinzani juu ya hilo, na watoto wenyewe nao walikuwa na hamu ya kushiriki vita hivyo. Hivyo ndivyo vikao vya dua na maombolezo vinavyoijenga jamii, na suala hilo ni moja kati ya misingi mikuu iliyojengwa na Uislamu tangu mwazo, kwa ajili ya kuihifadhi jamii ya Waislamu. Ni muhimu watu kuufahamu umuhimu wa maombolezo, na faida zinazopatikana ndani ya maombolezo hayo, pia wao wanatakiwa kufahamu kuwa: ni jambo gani hasa lenye kuvifanya vikao kama hivyo kuwa na umuhimu wa hali ya juu kama hiyo? Wale wajinga wangeliufahamu umuhimu na uhakika wa hilo, basi wasungetuita sisi kuwa ni (kaumu ya waliaji), bali wangelituita kuwa ni (kaumu ya wana hamasa). Watu wangeliufahamu uhakika wa dua za Imau Sajjaad (a.s) zilizomo ndani ya kitabu (Sahifatu-Sajjaadiyya), na vipi dua hizo zilivyoweza kuleta mageuzi mbali mbali ya Kisiasa, pia jinsi ya dua hizo zinavyoweza kumjenga mja kiimani na kifikra, basi wasingetuuliza sisi: ni kwa nini tosome dua? Kwani dua hizi zina umuhimu gani? Jamii yetu ni lazima ifahamu umuhimu wa vikao hivi, vikao hivi ndivyo vinavyoipa uhai jamii yetu na jamii za wenzetu. Enyi wanajamii msiache kusimamisha aina hii ya vikao, ndani ya Muharram, na msiache kusoma aina mbali mbali za dua ndani ya kila wiki, kwani watu wangelikuwa wanafahamu umuhimu wa dua na vikao hivyo! Basi hata wale waliojisinga (waliojipaka) rangi ya Umagharibi pia mngeliwaona wanahudhuria vikao vyenu, mimi nina matuaini kwa wanajamii wangu kuvitunza na kuvikozesha rangi zaidi vikao hivi… .[3] Mwisho wa kunukuu.
Kwa ajili ya kupata ufafanuzi zaidi kuhusiana na mada ya maombolezo ya Karbala, unaweza kuangalia vitabu husika vyenye kuzungumzia mada na faida za maombolezo ya Karbala.
[1] Sahifeye Imamu, juz/13, uk/326, chapa ya Tandhiim wa nashr aathaa Imamu Khomeiniy, Tehran, chapa ya nne ya mwaka 1386 Shamsia.
[2] Rejeo iliopita, juz/15, uk/330.
[3] Rejeo iliopita, juz/16, uk/344 hadi 348.